Skip to content
2 Wafalme 9:7-28

2 Wafalme 9:7-28

7
Inakupasa uiangamize nyumba ya bwana wako Ahabu, nami nitalipiza kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii na damu ya watumishi wote wa Bwana iliyomwagwa na Yezebeli.
8
Nyumba yote ya Ahabu itaangamia. Nitamkatilia mbali kila mzaliwa wa kiume wa Ahabu katika Israeli, aliye mtumwa ama aliye huru.
9
Nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama ile nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama ile nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.
10
Kuhusu Yezebeli, mbwa watamla kwenye kiwanja huko Yezreeli, wala hakuna mtu atakayemzika.’ ” Kisha akafungua mlango na kukimbia.
11
Yehu alipotoka nje na kurudi kwenda kwa maafisa wenzake, mmoja wao akamuuliza, “Je, kila kitu ni salama? Kwa nini huyu mwenye wazimu alikuja kwako?” Yehu akajibu, “Wewe unamfahamu huyo mtu, na aina ya mambo ambayo yeye husema.”
12
Wakasema, “Hiyo siyo kweli! Tuambie.” Yehu akasema, “Haya ndiyo aliyoniambia: ‘Hivi ndivyo asemavyo Bwana: Ninakutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli.’ ”
13
Wakaharakisha kuvua mavazi yao, na kuyatandaza chini ya Yehu ili akanyage juu kwenye ngazi ya nje. Kisha wakapiga tarumbeta na kupaza sauti wakisema, “Yehu ni mfalme!”
14
Basi Yehu mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya shauri baya dhidi ya Yoramu. (Wakati huu, Yoramu na Israeli wote walikuwa wakiilinda Ramoth-Gileadi dhidi ya Hazaeli mfalme wa Aramu,
15
lakini Mfalme Yoramu alikuwa amerudishwa Yezreeli ili kujiuguza kutokana na majeraha ambayo Waaramu walimtia katika vita na Hazaeli mfalme wa Aramu.) Yehu akasema, “Kama hii ndiyo nia yenu, msimruhusu hata mmoja kutoroka nje ya mji kwenda kupeleka habari huko Yezreeli.”
16
Ndipo Yehu akaingia katika gari lake la vita na kuendesha kwenda Yezreeli, kwa sababu Yoramu alikuwa amepumzika huko, na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameenda kumwona.
17
Mlinzi aliyesimama juu ya kinara cha Yezreeli alipoona askari wa Yehu wanakuja, akaita akisema, “Naona askari wanakuja.” Yoramu akaamuru, “Mtwae mpanda farasi umtume akakutane nao na kuuliza, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ”
18
Mpanda farasi akaondoka kwenda kukutana na Yehu na kusema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme: ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ” Yehu akamjibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.” Mlinzi akatoa habari, “Mjumbe amewafikia lakini harudi.”
19
Basi mfalme akamtuma mpanda farasi wa pili. Wakati alipowafikia akasema, “Hivi ndivyo asemavyo mfalme, ‘Je, mmekuja kwa amani?’ ” Yehu akajibu, “Una nini na amani? Unga msafara nyuma yangu.”
20
Yule mlinzi akatoa taarifa akasema, “Mjumbe amewafikia, lakini hata yeye harudi. Uendeshaji ule ni kama wa Yehu mwana wa Nimshi, anaendesha kama mwenye wazimu!”
21
Yoramu akaagiza, akasema, “Weka tayari gari langu la vita.” Na baada ya gari kuwa tayari, Yoramu mfalme wa Israeli, na Ahazia mfalme wa Yuda, wakaondoka kila mmoja kwenye gari lake ili kukutana na Yehu. Walikutana naye katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli.
22
Yoramu alipomwona Yehu akauliza, “Je, Yehu, umekuja kwa amani?” Yehu akajibu, “Kunawezaje kuwa na amani wakati ibada za sanamu na uchawi wa mama yako Yezebeli ungaliko?”
23
Yoramu akageuka nyuma na kukimbia, akimwambia Ahazia, “Huu ni uhaini, Ahazia!”
24
Kisha Yehu akatwaa upinde wake na kumchoma Yoramu katikati ya mabega. Mshale ukapenya kwenye moyo wake, naye akaanguka ghafula ndani ya gari lake.
25
Yehu akamwambia Bidkari, mwendeshaji wa gari lake, “Mwinue na umtupe katika shamba lililokuwa mali ya Nabothi, Myezreeli. Kumbuka jinsi mimi na wewe tulivyokuwa tukiendesha pamoja magari yetu nyuma ya Ahabu baba yake, wakati Bwana alipotoa unabii huu kumhusu:
26
‘Jana niliona damu ya Nabothi na damu ya wanawe, nami kwa hakika nitakufanya uilipe juu ya shamba hili, asema Bwana.’ Sasa basi, mwinue na umtupe juu ya kiwanja, kulingana na neno la Bwana.”
27
Wakati Ahazia mfalme wa Yuda alipoona kilichotokea, akakimbia kupitia barabara ya Beth-Hagani. Yehu akamkimbiza akipaza sauti na kusema, “Muue naye pia!” Wakamjeruhi katika gari lake kwenye njia ielekeayo Guri karibu na Ibleamu, lakini akatorokea Megido na akafia huko.
28
Watumishi wake wakambeba kwa gari la vita na kumpeleka Yerusalemu, wakamzika pamoja na baba zake kwenye kaburi lake katika Mji wa Daudi.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options