Skip to content
2 Wafalme 17:24-41

2 Wafalme 17:24-41

24
Mfalme wa Ashuru akawaleta watu kutoka Babeli, Kutha, Ava, Hamathi na Sefarvaimu na kuwaweka katika miji ya Samaria badala ya Waisraeli. Wakaimiliki Samaria na kuishi katika miji yake.
25
Wakati walianza kuishi humo, hawakumwabudu Bwana, kwa hiyo akatuma simba miongoni mwao, wakawaua baadhi ya watu.
26
Habari ikapelekwa kwa mfalme wa Ashuru, kusema: “Watu uliowahamisha na kuwaweka katika miji ya Samaria hawajui kile Mungu wa nchi hiyo anachokitaka. Ametuma simba miongoni mwao, ambao wanawaua, kwa sababu watu hawajui anachokitaka.”
27
Ndipo mfalme wa Ashuru akaamuru hivi: “Mtwae mmoja wa makuhani uliowachukua mateka kutoka Samaria ili arudi kuishi humo na awafundishe watu kile ambacho Mungu wa nchi anataka.”
28
Basi mmoja wa makuhani ambaye alikuwa amepelekwa uhamishoni kutoka Samaria akaja kuishi Betheli na kuwafundisha jinsi ya kumwabudu Bwana.
29
Hata hivyo, kila kikundi cha taifa lililoletwa Samaria kilitengeneza miungu yao wenyewe katika miji kadhaa mahali walipoishi, nao wakaiweka mahali pa ibada za miungu ambapo watu wa Samaria walikuwa wametengeneza katika mahali pa juu.
30
Watu kutoka Babeli wakamtengeneza Sukoth-Benothi kuwa mungu wao, watu kutoka Kutha wakamtengeneza Nergali, na watu kutoka Hamathi wakamtengeneza Ashima;
31
Waavi wakatengeneza Nibhazi na Tartaki, nao Wasefarvi wakachoma watoto wao kama kafara kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.
32
Walimwabudu Bwana, lakini pia waliteua aina zote za watu wao ili kuwawakilisha kama makuhani katika mahali pa kuabudia miungu kwenye mahali pa juu pa ibada.
33
Walimwabudu Bwana, lakini pia waliitumikia miungu yao kulingana na desturi za mataifa walikotoka.
34
Mpaka leo wanashikilia desturi zao za zamani. Hawamwabudu Bwana wala kuzishika hukumu na maagizo, sheria na amri ambazo Bwana aliwapa uzao wa Yakobo, ambaye alimwita Israeli.
35
Wakati Bwana alipofanya Agano na Waisraeli, aliwaamuru akisema: “Msiiabudu miungu mingine yoyote wala kuisujudia, wala kuitumikia wala kuitolea dhabihu.
36
Bali imewapasa kumwabudu Bwana aliyewapandisha kutoka Misri kwa uwezo wake mkuu na kwa mkono wake ulionyooshwa. Kwake yeye mtasujudu na kwake yeye mtatoa dhabihu.
37
Imewapasa daima kuwa waangalifu kutunza hukumu na maagizo, sheria na amri alizowaandikia. Msiabudu miungu mingine.
38
Msisahau agano nililofanya nanyi, wala msiabudu miungu mingine.
39
Bali, mtamwabudu Bwana Mungu wenu, kwani yeye ndiye atakayewakomboa kutoka mikononi mwa adui zenu wote.”
40
Hata hivyo hawakusikiliza, lakini waliendelea na desturi zao za awali.
41
Hata wakati watu hawa walipokuwa wanamwabudu Bwana, walikuwa bado wakitumikia sanamu zao. Mpaka leo watoto wao na watoto wa watoto wao wanaendelea kufanya kama baba zao walivyofanya.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options