2 Nyakati 9:13-28
13
Uzito wa dhahabu ambayo Solomoni alipokea kwa mwaka ulikuwa talanta 666,
14
mbali na mapato yaliyoletwa na wafanyabiashara na wachuuzi. Wafalme wote wa Arabuni na watawala wa nchi wakamletea Solomoni dhahabu na fedha.
15
Mfalme Solomoni akatengeneza ngao kubwa 200 kwa dhahabu iliyofuliwa. Kila ngao ilikuwa na dhahabu yenye uzito wa shekeli 600
16
Akatengeneza pia ngao ndogo 300 za dhahabu iliyofuliwa, kila ngao ikiwa na uzito wa mane tatu za dhahabu. Mfalme akaziweka katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni.
17
Kisha mfalme akatengeneza kiti kikubwa cha kifalme kwa kutumia pembe za ndovu na kukifunika kwa dhahabu safi.
18
Kiti hicho kilikuwa na ngazi sita na mahali pa kuwekea miguu vyote vya dhahabu. Pande zote za kiti kulikuwa na mahali pa kuegemeza mikono, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.
19
Simba kumi na wawili walisimama kwenye ngazi sita, mmoja katika kila upande wa kila ngazi. Hakuna kitu kama hicho kilichokuwa kimefanyika kwenye ufalme mwingine wowote.
20
Vikombe vyote vya Mfalme Solomoni vya kunywea vilikuwa vya dhahabu na vyombo vyote vya nyumbani katika Jumba la Kifalme la Msitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu safi. Hakukuwa na kitu kilichotengenezwa kwa fedha, kwa sababu fedha ilionekana ya thamani ndogo wakati wa Solomoni.
21
Mfalme alikuwa na meli nyingi za biashara baharini zilizoendeshwa na watu wa Hiramu. Kwa mara moja kila miaka mitatu zilirudi, zikiwa zimebeba dhahabu, fedha, pembe za ndovu na nyani wakubwa na wadogo.
22
Mfalme Solomoni alikuwa mkuu zaidi kwa utajiri na hekima kuliko wafalme wote wa dunia.
23
Wafalme wote wa dunia wakatafuta kukutana na Solomoni ili kusikia hekima ambayo Mungu alikuwa ameiweka katika moyo wake.
24
Mwaka baada ya mwaka, kila mmoja ambaye alikuja, alileta zawadi, vyombo vya fedha na dhahabu, majoho, silaha na vikolezi, farasi na nyumbu.
25
Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 kwa ajili ya farasi na magari ya vita, farasi 12,000 ambao aliwaweka katika miji ya magari ya vita na katika Yerusalemu pamoja naye.
26
Solomoni akatawala juu ya wafalme wote kuanzia Mto Frati mpaka kwenye nchi ya Wafilisti na kuendelea hadi mpaka wa Misri.
27
Mfalme akafanya fedha kuwa kitu cha kawaida kama mawe huko Yerusalemu, mierezi akaifanya kuwa mingi kama mikuyu vilimani.
28
Farasi wa Solomoni waliletwa kutoka Misri na kutoka nchi nyingine zote.
Settings