Skip to content
2 Nyakati 29:22-36

2 Nyakati 29:22-36

22
Hivyo wakachinja wale mafahali, nao makuhani wakachukua ile damu na kuinyunyiza kwenye madhabahu, halafu wakawachinja wale kondoo dume saba na kunyunyiza hiyo damu yao kwenye madhabahu, kisha wakawachinja wale wana-kondoo dume na kunyunyiza damu yao kwenye madhabahu.
23
Wale mabeberu waliokuwa kwa ajili ya sadaka ya dhambi wakaletwa mbele ya mfalme na kusanyiko nao wakaweka mikono yao juu hao mabeberu.
24
Ndipo makuhani wakawachinja hao mabeberu na kuweka damu yao kwenye madhabahu kwa ajili ya sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli yote, kwa sababu mfalme alikuwa ameamuru hiyo sadaka ya kuteketezwa na hiyo sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli yote.
25
Akawaweka Walawi kwenye Hekalu la Bwana wakiwa na matoazi, vinubi na zeze kama ilivyoagizwa na Daudi na Gadi mwonaji wa mfalme pamoja na nabii Nathani kwani hili lilikuwa limeamriwa na Bwana kupitia manabii wake.
26
Hivyo Walawi wakasimama tayari wakiwa na ala za uimbaji za Daudi na makuhani walikuwa na tarumbeta zao.
27
Hezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbia Bwana pamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli.
28
Kusanyiko lote wakaabudu kwa kusujudu, wakati waimbaji wakiwa wanaimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea mpaka walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.
29
Kutoa sadaka kulipomalizika, mfalme na kila mtu aliyekuwepo pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu.
30
Mfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifu Bwana kwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.
31
Kisha Hezekia akasema, “Sasa mmejiweka wakfu kwa Bwana. Njooni mlete dhabihu na sadaka za shukrani Hekaluni mwa Bwana.” Hivyo kusanyiko likaleta dhabihu na sadaka za shukrani, nao wote waliokuwa na mioyo ya hiari wakaleta sadaka za kuteketezwa.
32
Idadi ya sadaka za kuteketezwa zilizoletwa na kusanyiko zilikuwa mafahali sabini, kondoo dume 100 na wana-kondoo dume 200. Wote hawa walikuwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa kwa Bwana.
33
Wanyama waliowekwa wakfu kwa sadaka ya kuteketezwa walikuwa mafahali 600, pamoja na kondoo na mbuzi 3,000.
34
Lakini makuhani walikuwa wachache sana kuweza kuchuna wale wanyama wote wa sadaka za kuteketezwa, kwa hiyo ndugu zao Walawi wakawasaidia mpaka kazi ile ikakamilika na mpaka makuhani wengine walipowekwa wakfu, kwa kuwa Walawi walikuwa makini kujiweka wakfu kuliko walivyokuwa makuhani.
35
Kulikuwa na sadaka nyingi za kuteketezwa, pamoja na mafuta ya wanyama ya sadaka za amani na sadaka za kinywaji ambazo ziliambatana na sadaka za kuteketezwa. Kwa hiyo huduma ya Hekalu la Bwana ikarudishwa kwa upya.
36
Hezekia pamoja na watu wote wakafurahi kwa sababu ya lile Mungu alilolifanya kwa ajili ya watu wake, kwa kuwa lilitendeka papo hapo.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 45 chars

Options