2 Nyakati 29:20-30
20
Ndipo Mfalme Hezekia akainuka asubuhi na mapema, akakusanya pamoja maafisa wa mji wakakwea hekaluni mwa Bwana.
21
Wakaleta mafahali saba, kondoo dume saba, wana-kondoo dume saba na mabeberu saba kuwa sadaka ya dhambi kwa ajili ya ufalme, kwa ajili ya mahali patakatifu na kwa ajili ya Yuda. Mfalme akawaamuru makuhani, wazao wa Aroni, kuvitoa vitu hivyo sadaka katika madhabahu ya Bwana.
22
Hivyo wakachinja wale mafahali, nao makuhani wakachukua ile damu na kuinyunyiza kwenye madhabahu, halafu wakawachinja wale kondoo dume saba na kunyunyiza hiyo damu yao kwenye madhabahu, kisha wakawachinja wale wana-kondoo dume na kunyunyiza damu yao kwenye madhabahu.
23
Wale mabeberu waliokuwa kwa ajili ya sadaka ya dhambi wakaletwa mbele ya mfalme na kusanyiko nao wakaweka mikono yao juu hao mabeberu.
24
Ndipo makuhani wakawachinja hao mabeberu na kuweka damu yao kwenye madhabahu kwa ajili ya sadaka ya dhambi ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Israeli yote, kwa sababu mfalme alikuwa ameamuru hiyo sadaka ya kuteketezwa na hiyo sadaka ya dhambi kwa ajili ya Israeli yote.
25
Akawaweka Walawi kwenye Hekalu la Bwana wakiwa na matoazi, vinubi na zeze kama ilivyoagizwa na Daudi na Gadi mwonaji wa mfalme pamoja na nabii Nathani kwani hili lilikuwa limeamriwa na Bwana kupitia manabii wake.
26
Hivyo Walawi wakasimama tayari wakiwa na ala za uimbaji za Daudi na makuhani walikuwa na tarumbeta zao.
27
Hezekia akatoa amri ya kutoa sadaka ya kuteketezwa madhabahuni. Walipoanza kutoa sadaka, wakaanza pia kumwimbia Bwana pamoja na tarumbeta na zile ala za uimbaji za Daudi mfalme wa Israeli.
28
Kusanyiko lote wakaabudu kwa kusujudu, wakati waimbaji wakiwa wanaimba na wenye tarumbeta wakipiga tarumbeta zao. Yote haya yaliendelea mpaka walipomaliza kutoa ile dhabihu ya sadaka ya kuteketezwa.
29
Kutoa sadaka kulipomalizika, mfalme na kila mtu aliyekuwepo pamoja naye wakapiga magoti na kuabudu.
30
Mfalme Hezekia na maafisa wake wakawaamuru Walawi kumsifu Bwana kwa maneno ya Daudi na ya Asafu mwonaji. Hivyo wakaimba sifa kwa furaha nao wakainamisha vichwa vyao na kuabudu.
Settings