1 Samweli 9:12-19
12
Wakajibu, “Yuko, yu mbele yenu amewatangulia, sasa fanyeni haraka, ndiyo tu amekuja mjini kwetu leo, kwa kuwa watu wana dhabihu huko mahali pa juu.
13
Mara tu mwingiapo mjini, mtamkuta kabla hajapanda kwenda mahali pa juu kula. Watu hawataanza kula mpaka atakapofika kwa sababu ni lazima kwanza yeye abariki dhabihu, ndipo wale walioalikwa watakapokula. Pandeni sasa, mtamkuta kwa wakati huu.”
14
Wakapanda mjini, nao walipokuwa wakiingia mjini, tazama, Samweli alikuwa akija kuelekea walikokwenda mahali pa juu.
15
Basi siku moja kabla Sauli hajaja, Bwana alikuwa amemfunulia Samweli jambo hili:
16
“Kesho wakati kama huu nitakupelekea mtu kutoka nchi ya Benyamini. Umtie mafuta awe kiongozi juu ya watu wangu Israeli, ndiye atakayewakomboa watu wangu na mkono wa Wafilisti. Nimewaangalia watu wangu, kwa kuwa kilio chao kimenifikia.”
17
Samweli alipomwona Sauli, Bwana akamwambia, “Huyu ndiye mtu niliyekuambia habari zake, kwamba yeye atawatawala watu wangu.”
18
Sauli akamkaribia Samweli langoni na kumuuliza, “Tafadhali, je, waweza kuniambia mahali nyumba ya mwonaji ilipo?”
19
Samweli akamjibu Sauli, “Mimi ndiye mwonaji, panda utangulie mbele yangu mpaka mahali pa juu, kwa kuwa leo itakupasa kula pamoja nami na asubuhi nitakuruhusu uende na nitakuambia yale yote yaliyo moyoni mwako.
Settings