1 Samweli 18:17-25
17
Sauli akamwambia Daudi, “Huyu hapa binti yangu mkubwa Merabu. Nitakupa umwoe, endapo tu utanitumikia kwa ushujaa na kupigana vita vya Bwana.” Kwa maana Sauli alisema moyoni mwake, “Sitainua mkono wangu dhidi yake. Acha mkono wa Wafilisti uwe juu yake.”
18
Lakini Daudi akamwambia Sauli, “Mimi ni nani, nayo jamaa yangu ni nini au ukoo wa baba yangu katika Israeli, kwamba mimi niwe mkwewe mfalme?”
19
Basi ulipofika wakati wa Daudi kupewa Merabu, binti Sauli, huyo binti aliozwa kwa Adrieli, Mmeholathi.
20
Basi Mikali binti Sauli alimpenda Daudi, nao walipomwambia Sauli juu ya jambo hili, likampendeza.
21
Sauli akawaza, “Nitampa Daudi binti yangu, ili apate kuwa mtego kwake, ili kwamba mkono wa Wafilisti upate kuwa juu yake.” Hivyo Sauli akamwambia Daudi, “Sasa unayo nafasi ya pili ya kuwa mkwe wangu.”
22
Ndipo Sauli akawaagiza watumishi wake, akisema, “Zungumzeni na Daudi kwa siri na kumwambia, ‘Tazama, mfalme amependezwa nawe, nao watumishi wake wote wanakupenda. Basi na uwe mkwewe mfalme.’ ”
23
Watumishi wa Sauli wakarudia hayo maneno kwa Daudi. Lakini Daudi akasema, “Je, mnafikiri ni jambo dogo kuwa mkwewe mfalme? Mimi ni mtu maskini tu, na nisiyejulikana sana.”
24
Watumishi wa Sauli walipomweleza yale Daudi aliyoyasema,
25
Sauli akajibu, “Mwambieni Daudi, ‘Mfalme hataki zawadi nyingine kuwa mahari isipokuwa magovi 100 ya Wafilisti, ili kulipiza kisasi juu ya adui zake.’ ” Mawazo ya Sauli yalikuwa Daudi akaanguke mikononi mwa Wafilisti.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings