1 Wafalme 13:11-22
11
Basi kulikuwepo na nabii fulani mzee aliyekuwa anaishi Betheli, ambaye wanawe walikuja kumwambia yote ambayo mtu wa Mungu alikuwa ameyafanya pale siku ile. Pia wakamwambia baba yao yale aliyomwambia mfalme.
12
Baba yao akawauliza, “Ameelekea njia gani?” Nao wanawe wakamwonyesha ile njia yule mtu wa Mungu kutoka Yuda aliyopita.
13
Hivyo akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda.” Walipokwisha kumtandikia punda, akampanda
14
na kumfuatilia yule mtu wa Mungu. Akamkuta ameketi chini ya mwaloni na akamuuliza, “Je, wewe ndiwe mtu wa Mungu kutoka Yuda?” Akamjibu, “Mimi ndiye.”
15
Basi nabii akamwambia, “Karibu nyumbani pamoja na mimi ule.”
16
Yule mtu wa Mungu akasema, “Siwezi kurudi na kwenda nawe, wala siwezi kula mkate au kunywa maji pamoja nawe mahali hapa.
17
Nimeambiwa kwa neno la Bwana: ‘Kamwe usile mkate au kunywa maji huko au kurudia njia uliyojia.’ ”
18
Yule nabii mzee akajibu, “Mimi pia ni nabii, kama wewe. Naye malaika alisema nami kwa neno la Bwana: ‘Mrudishe aje katika nyumba yako ili apate kula mkate na kunywa maji.’ ” (Lakini alikuwa akimwambia uongo.)
19
Hivyo mtu wa Mungu akarudi pamoja naye na akala na kunywa katika nyumba yake.
20
Wakati walipokuwa wameketi mezani, neno la Bwana likamjia yule nabii mzee aliyemrudisha huyo mtu wa Mungu.
21
Akampazia sauti yule mtu wa Mungu aliyekuwa ametoka Yuda, “Hivi ndivyo asemavyo Bwana: ‘Umeasi neno la Bwana na hukushika amri uliyopewa na Bwana Mungu wako,
22
bali ulirudi na ukala mkate na kunywa maji mahali ambapo alikuambia usile wala usinywe. Kwa hiyo maiti yako haitazikwa katika kaburi la baba zako.’ ”
Settings