1 Wafalme 13:23-32
23
Wakati huyo mtu wa Mungu alipomaliza kula na kunywa, nabii aliyekuwa amemrudisha akamtandikia punda wake.
24
Alipokuwa akienda akakutana na simba njiani, akamuua na maiti yake ikabwagwa barabarani, yule punda wake na simba wakiwa wamesimama karibu yake.
25
Baadhi ya watu waliopita pale waliona maiti imebwagwa pale chini, simba akiwa amesimama kando ya maiti, wakaenda na kutoa habari katika mji ambao nabii mzee aliishi.
26
Yule nabii aliyekuwa amemrudisha kutoka safari yake aliposikia habari hii akasema, “Ni yule mtu wa Mungu ambaye aliasi neno la Bwana. Bwana amemtoa kwa simba, ambaye amemrarua na kumuua, sawasawa na neno la Bwana lilivyokuwa limemwonya.”
27
Nabii akawaambia wanawe, “Nitandikieni punda,” nao wakafanya hivyo.
28
Kisha akatoka akaenda akakuta maiti imebwagwa chini barabarani, punda na simba wakiwa wamesimama kando yake. Simba hakuwa amekula ile maiti wala kumrarua punda.
29
Basi yule nabii mzee akachukua maiti ya mtu wa Mungu, akailaza juu ya punda na akairudisha katika mji wake, ili amwombolezee na kumzika.
30
Kisha akailaza ile maiti katika kaburi lake huyo nabii mzee, nao wakaomboleza juu yake na kusema, “Ee ndugu yangu!”
31
Baada ya kumzika, akawaambia wanawe, “Wakati nitakapokufa, mnizike kwenye kaburi alimozikwa huyu mtu wa Mungu; lazeni mifupa yangu kando ya mifupa yake.
32
Kwa maana ujumbe alioutangaza kwa neno la Bwana dhidi ya madhabahu huko Betheli na dhidi ya madhabahu yote katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Samaria, hakika yatatokea kweli.”
Settings