1 Nyakati 22:6-16
6
Kisha akamwita Solomoni mwanawe akamwagiza kujenga nyumba kwa ajili ya Bwana, Mungu wa Israeli.
7
Daudi akamwambia Solomoni: “Mwanangu, nilikuwa na jambo hili ndani ya moyo wangu kujenga nyumba kwa ajili ya Jina la Bwana Mungu wangu.
8
Lakini neno hili la Bwana likanijia, kusema: ‘Wewe umemwaga damu nyingi na kupigana vita vingi. Wewe hutajenga nyumba kwa ajili ya Jina langu, kwa sababu umemwaga damu nyingi juu ya nchi machoni pangu.
9
Lakini utakuwa na mwana ambaye atakuwa mtu wa amani na utulivu nami nitampa utulivu mbele ya adui zake wote pande zote. Jina lake ataitwa Solomoni, nami nitawapa Israeli amani na utulivu wakati wa utawala wake.
10
Yeye ndiye atakayejenga nyumba kwa ajili ya Jina langu. Yeye atakuwa mwanangu, nami nitakuwa baba yake. Nami nitakifanya imara kiti chake cha enzi cha utawala wake katika Israeli milele.’
11
“Sasa, mwanangu, Bwana awe pamoja nawe, nawe uwe na mafanikio upate kuijenga nyumba ya Bwana Mungu wako, kama alivyosema utafanya.
12
Bwana na akupe hekima na ufahamu wakati atakuweka juu ya Israeli, ili uweze kuishika sheria ya Bwana Mungu wako.
13
Ndipo utakapofanikiwa, ikiwa utakuwa na bidii kutii amri na sheria Bwana alizompa Mose kwa ajili ya Israeli. Uwe hodari na ushujaa. Usiogope wala usikate tamaa.
14
“Nimejitaabisha sana ili kupata mahitaji kwa ajili ya Hekalu la Bwana: talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na kiasi kisichopimika cha shaba na chuma, pia mbao na mawe. Nawe waweza kuviongeza.
15
Unao wafanyakazi wengi: Wachonga mawe, waashi na maseremala, pamoja na watu walio na ustadi katika kila kazi
16
wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma, mafundi wasiohesabika. Sasa basi anza kazi hii, naye Bwana awe pamoja nawe.”
Settings