Rukia maudhui

Zaburi90

Mungu, Kimbilio Letu la Milele

1
Maombi ya Mose, mtu wa Mungu. Bwana, wewe umekuwa makao yetu katika vizazi vyote.
2
Kabla ya kuzaliwa milima au hujaumba dunia na ulimwengu, wewe ni Mungu tangu milele hata milele.

Ufupi wa Maisha ya Mwanadamu

3
Huwarudisha watu mavumbini, ukisema, “Rudini mavumbini, enyi wanadamu.”
4
Kwa maana kwako miaka elfu ni kama siku moja iliyokwisha pita, au kama kesha la usiku.
5
Unawatowesha wanadamu katika usingizi wa kifo, nao ni kama majani machanga ya asubuhi:
6
ingawa asubuhi yanachipua, ifikapo jioni huwa yamenyauka na kukauka.

Kufa kwa Mwanadamu kwa Sababu ya Dhambi

7
Tumeangamizwa kwa hasira yako na tumetishwa kwa ghadhabu yako.
8
Umeyaweka maovu yetu mbele yako, dhambi zetu za siri katika nuru ya uwepo wako.
9
Tumeishi siku zetu zote chini ya ghadhabu yako, tunamaliza miaka yetu kwa kuomboleza.
10
Siku zetu za kuishi ni miaka sabini, au miaka themanini ikiwa tuna nguvu, lakini yote ni ya shida na taabu, nazo zapita haraka, nasi twatoweka.
11
Ni nani ajuaye nguvu za hasira yako? Kwa maana ghadhabu yako ni kubwa kama hofu tunayopaswa kuwa nayo kwako.

Sala ya Hekima na Rehema

12
Tufundishe kuzihesabu siku zetu vizuri, ili tujipatie moyo wa hekima.
13
Ee Bwana, uwe na huruma! Utakawia hata lini? Wahurumie watumishi wako.
14
Tushibishe asubuhi kwa upendo wako usiokoma, ili tuweze kuimba kwa shangwe na kufurahi siku zetu zote.
15
Utufurahishe kulingana na siku ulizotuadhibu, kulingana na miaka tuliyotaabika.
16
Matendo yako na yaonekane kwa watumishi wako, utukufu wako kwa watoto wao.
17
Wema wa Bwana Mungu wetu uwe juu yetu; uzithibitishe kazi za mikono yetu: naam, uzithibitishe kazi za mikono yetu.
Use arrow keys to navigate
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 45 chars

Options