Rukia maudhui

circa 970–930 BC

Solomon & The Temple

Solomon builds the great Temple in Jerusalem and rules with unprecedented wisdom and wealth before foreign gods divide his heart.

635 mistari · 2 vitabu vimehusishwa

Mistari ya kipindi hiki

Chuja kwa kitabu
  1. 1 Wafalme 3:2takriban 1014 KK

    Hata hivyo, watu bado walikuwa wakitoa dhabihu huko kwenye vilima, kwa sababu Hekalu lilikuwa bado halijajengwa kwa ajili ya Jina la Bwana.

  2. 1 Wafalme 3:3takriban 1014 KK

    Solomoni akaonyesha upendo wake kwa Bwana kwa kuenenda sawasawa na amri za Daudi baba yake, ila yeye alitoa dhabihu na kufukiza uvumba huko mahali pa juu.

  3. 1 Wafalme 3:4takriban 1014 KK

    Mfalme akaenda Gibeoni kutoa dhabihu, kwa maana ndipo palipokuwa mahali pa juu pa kuabudia, naye Solomoni akatoa sadaka elfu moja za kuteketezwa juu ya hayo madhabahu.

  4. 1 Wafalme 3:5takriban 1014 KK

    Bwana akamtokea Solomoni huko Gibeoni wakati wa usiku katika ndoto, naye Mungu akasema, “Omba lolote utakalo nikupe.”

  5. 1 Wafalme 3:6takriban 1014 KK

    Solomoni akajibu, “Umemfanyia mtumishi wako, baba yangu Daudi, fadhili nyingi, kwa kuwa alikuwa mwaminifu kwako na mwenye haki, tena mnyofu wa moyo. Nawe umemzidishia fadhili hii kuu kwani umempa mwana wa kuketi kwenye kiti chake cha ufalme, kama ilivyo leo.

  6. 1 Wafalme 3:7takriban 1014 KK

    “Sasa, Ee Bwana Mungu wangu, umemfanya mtumishi wako mfalme badala ya baba yangu Daudi. Lakini mimi ni mtoto mdogo tu, wala sijui jinsi ya kutekeleza wajibu wangu.

  7. 1 Wafalme 3:8takriban 1014 KK

    Mtumishi wako yuko hapa miongoni mwa watu uliowachagua: taifa kubwa, watu wengi wasioweza kuhesabika wala kutoa idadi yao.

  8. 1 Wafalme 3:9takriban 1014 KK

    Hivyo mpe mtumishi wako moyo wa ufahamu ili kutawala watu wako na kupambanua kati ya mema na mabaya. Kwa maana, ni nani awezaye kutawala watu wako hawa walio wengi hivi?”

  9. 1 Wafalme 3:10takriban 1014 KK

    Bwana akapendezwa kwamba Solomoni ameliomba jambo hili.

  10. 1 Wafalme 3:11takriban 1014 KK

    Basi Mungu akamwambia, “Kwa kuwa umeomba neno hili na hukuomba maisha marefu au upate utajiri kwa nafsi yako, wala adui zako wafe, bali umeomba ufahamu katika kutoa haki,

  11. 1 Wafalme 3:12takriban 1014 KK

    nitafanya lile uliloomba. Nitakupa moyo wa hekima na wa ufahamu, kiasi kwamba hajakuwepo mtu mwingine kama wewe, wala kamwe hatakuwepo baada yako.

  12. 1 Wafalme 3:13takriban 1014 KK

    Zaidi ya hayo, nitakupa yale ambayo hukuomba, yaani utajiri na heshima, ili kwamba maisha yako yote hapatakuwa na mtu kama wewe miongoni mwa wafalme.

  13. 1 Wafalme 3:14takriban 1014 KK

    Nawe kama ukienenda katika njia zangu na kutii sheria na amri zangu kama baba yako Daudi alivyofanya, nitakupa maisha marefu.”

  14. 1 Wafalme 3:15takriban 1014 KK

    Ndipo Solomoni akaamka, akatambua kuwa ilikuwa ndoto. Akarudi Yerusalemu, akasimama mbele ya Sanduku la Agano la Bwana, naye akatoa dhabihu za kuteketezwa na sadaka za amani. Kisha akawafanyia watumishi wake wote karamu.

  15. 1 Wafalme 3:16takriban 1014 KK

    Basi wanawake wawili makahaba walikuja kwa mfalme na kusimama mbele yake.

  16. 1 Wafalme 3:17takriban 1014 KK

    Mmojawapo akasema, “Bwana wangu, mimi na mwanamke huyu tunaishi kwenye nyumba moja. Nilikuwa nimezaa alipokuwa pamoja nami.

  17. 1 Wafalme 3:18takriban 1014 KK

    Siku ya tatu baada ya mtoto wangu kuzaliwa, mwanamke huyu pia naye akazaa mtoto. Tulikuwa peke yetu, hapakuwa na mtu mwingine yeyote katika nyumba isipokuwa sisi wawili.

  18. 1 Wafalme 3:19takriban 1014 KK

    “Wakati wa usiku mwana wa huyu mwanamke akafa kwa sababu alimlalia.

  19. 1 Wafalme 3:20takriban 1014 KK

    Hivyo akaondoka katikati ya usiku na kumchukua mwanangu kutoka ubavuni pangu wakati mimi mtumishi wako nilipokuwa nimelala. Akamweka kifuani mwake na kumweka mwanawe aliyekufa kifuani mwangu.

  20. 1 Wafalme 3:21takriban 1014 KK

    Asubuhi yake, nikaamka ili kumnyonyesha mwanangu, naye alikuwa amekufa! Lakini nilipomwangalia sana katika nuru ya asubuhi, niliona kuwa hakuwa yule mwana niliyekuwa nimemzaa.”

  21. 1 Wafalme 3:22takriban 1014 KK

    Huyo mwanamke mwingine akasema, “Hapana! Mwana aliye hai ndiye wangu, aliyekufa ni wako.” Lakini yule wa kwanza akasisitiza, “Hapana! Mwana aliyekufa ni wako, aliye hai ni wangu.” Hivi ndivyo walivyobishana mbele ya mfalme.

  22. 1 Wafalme 3:23takriban 1014 KK

    Mfalme akasema, “Huyu anasema, ‘Mwanangu ndiye aliye hai, na aliyekufa ndiye mwanao,’ maadamu yule anasema, ‘Hapana! Aliyekufa ni wako, na aliye hai ni wangu.’ ”

  23. 1 Wafalme 3:24takriban 1014 KK

    Kisha mfalme akasema, “Nileteeni upanga.” Basi wakamletea mfalme upanga.

  24. 1 Wafalme 3:25takriban 1014 KK

    Ndipo mfalme akatoa amri: “Mkate mtoto aliye hai vipande viwili; mpe huyu nusu na mwingine nusu.”

  25. 1 Wafalme 3:26takriban 1014 KK

    Mwanamke ambaye mwanawe alikuwa hai akajawa na huruma kwa ajili ya mwanawe na kumwambia mfalme, “Tafadhali, bwana wangu, mpe yeye mtoto aliye hai! Usimuue!” Lakini yule mwanamke mwingine akasema, “Mkate vipande viwili. Asiwe wangu au wake!”