Nehemia 12:27-43
27
Wakati wa kuwekwa wakfu ukuta wa Yerusalemu, Walawi walitafutwa kule walikokuwa wakiishi, nao wakaletwa Yerusalemu kuadhimisha kwa shangwe huko kuweka wakfu kwa nyimbo za shukrani na kwa uimbaji wakitumia matoazi, vinubi na zeze.
28
Pia waimbaji walikusanywa pamoja kutoka maeneo yaliyozunguka Yerusalemu, kutoka vijiji vya Wanetofathi,
29
kutoka Beth-Gilgali, na kutoka eneo la Geba na Azmawethi, kwa kuwa waimbaji walikuwa wamejijengea vijiji kuzunguka Yerusalemu.
30
Wakati makuhani na Walawi walipokuwa wamekwisha kujitakasa kwa kufuatana na desturi, waliwatakasa watu, malango na ukuta.
31
Niliwaagiza viongozi wa Yuda wapande juu ya ukuta. Pia niliagiza makundi mawili makubwa ya waimbaji waimbe nyimbo za kumshukuru Mungu. Kundi moja lilipanda juu ya ukuta upande wa kuume, kuelekea Lango la Samadi.
32
Hoshaya na nusu ya viongozi wa Yuda wakawafuata,
33
pamoja na Azaria, Ezra, Meshulamu,
34
Yuda, Benyamini, Shemaya, Yeremia,
35
pamoja na baadhi ya makuhani wenye tarumbeta, na pia walikuwa na Zekaria mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu,
36
pamoja na wenzake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda na Hanani, wakiwa na vyombo vya uimbaji, kama ilivyoagizwa na Daudi mtu wa Mungu. Mwandishi Ezra aliongoza maandamano.
37
Kwenye Lango la Chemchemi waliendelea moja kwa moja mpaka kwenye ngazi za Mji wa Daudi, kwenye mwinuko wa ukuta, na kupitia juu ya nyumba ya Daudi mpaka kwenye Lango la Maji upande wa mashariki.
38
Kundi la pili la waimbaji lilielekea upande wa kushoto. Niliwafuata juu ya ukuta, pamoja na nusu ya watu kupitia Mnara wa Tanuru mpaka kwenye Ukuta Mpana,
39
juu ya Lango la Efraimu, Lango la Yeshana, Lango la Samaki, Mnara wa Hananeli, na Mnara wa Mia, mpaka kwenye Lango la Kondoo. Walipofika kwenye Lango la Ulinzi wakasimama.
40
Kisha yale makundi mawili ya waimbaji yaliyoshukuru yakachukua nafasi zao katika nyumba ya Mungu. Nami pia nikafanya hivyo, pamoja na nusu ya maafisa,
41
na makuhani wafuatao: Eliakimu, Maaseya, Miniamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania wakiwa na tarumbeta zao,
42
na pia Maaseya, Shemaya, Eleazari, Uzi, Yehohanani, Malkiya, Elamu na Ezeri. Makundi haya yaliimba chini ya uongozi wa Yezrahia.
43
Siku hiyo watu walitoa dhabihu nyingi, wakishangilia kwa sababu Mungu aliwapa furaha kuu. Wanawake na watoto walishangilia pia. Sauti ya kushangilia huko Yerusalemu iliweza kusikika mbali sana.
Settings