Mathayo 17:1-19
1
Siku sita baada ya jambo hili, Yesu akawachukua Petro, Yakobo na Yohana ndugu yake Yakobo, akawapeleka juu ya mlima mrefu peke yao.
2
Wakiwa huko, Yesu alibadilika sura mbele yao. Uso wake ukangʼaa kama jua na nguo zake zikawa na weupe wa kuumiza macho.
3
Ghafula wakawatokea mbele yao Mose na Eliya, wakizungumza na Yesu.
4
Ndipo Petro akamwambia Yesu, “Bwana, ni vyema sisi tukae hapa. Ukitaka, nitafanya vibanda vitatu: kimoja chako, kingine cha Mose na kingine cha Eliya.”
5
Petro alipokuwa angali ananena, ghafula wingu lililongʼaa likawafunika, na sauti ikatoka kwenye hilo wingu ikisema, “Huyu ni Mwanangu mpendwa. Ninapendezwa naye sana. Msikieni yeye.”
6
Wanafunzi waliposikia haya, wakaanguka chini kifudifudi, wakajawa na hofu.
7
Lakini Yesu akaja na kuwagusa, akawaambia, “Inukeni na wala msiogope.”
8
Walipoinua macho yao, hawakumwona mtu mwingine yeyote isipokuwa Yesu.
9
Walipokuwa wakishuka kutoka mlimani, Yesu akawaagiza, “Msimwambie mtu yeyote mambo mliyoyaona hapa, mpaka Mwana wa Adamu atakapofufuliwa kutoka kwa wafu.”
10
Wale wanafunzi wakamuuliza, “Kwa nini basi walimu wa sheria husema kwamba ni lazima Eliya aje kwanza?”
11
Yesu akawajibu, “Ni kweli, Eliya lazima aje kwanza, naye atatengeneza mambo yote.
12
Lakini nawaambia, Eliya amekwisha kuja, nao hawakumtambua, bali walimtendea kila kitu walichotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu pia atateswa mikononi mwao.”
13
Ndipo wale wanafunzi wakaelewa kuwa alikuwa anazungumza nao habari za Yohana Mbatizaji.
14
Walipofika penye umati wa watu, mtu mmoja akamjia Yesu na kupiga magoti mbele yake, akasema,
15
“Bwana, mhurumie mwanangu. Yeye ana kifafa na anateseka sana. Mara kwa mara huanguka kwenye moto au kwenye maji.
16
Nilimleta kwa wanafunzi wako, lakini hawakuweza kumponya.”
17
Yesu akajibu, “Enyi kizazi kisichoamini na kilichopotoka! Nitakaa nanyi mpaka lini? Nitawavumilia mpaka lini? Mleteni mvulana hapa kwangu.”
18
Yesu akamkemea yule pepo mchafu, akamtoka yule kijana, naye akapona saa ile ile.
19
Kisha wanafunzi wakamwendea Yesu wakiwa peke yao, wakamuuliza, “Kwa nini sisi hatukuweza kumtoa?”
Settings