Waamuzi 1:21-36
21
Hata hivyo, Wabenyamini walishindwa kuwafukuza Wayebusi, waliokuwa wanaishi Yerusalemu; hivyo hadi leo Wayebusi huishi humo pamoja na Wabenyamini.
22
Basi nyumba ya Yosefu wakashambulia Betheli, naye Bwana alikuwa pamoja nao.
23
Walipotuma watu kwenda kupeleleza Betheli (ambao hapo kwanza uliitwa Luzu),
24
wale wapelelezi wakaona mtu anatoka mjini, nao wakamwambia, “Tuonyeshe jinsi ya kuingia mjini nasi tutakutendea wema.”
25
Hivyo akawaonyesha, nao wakaupiga mji kwa upanga lakini wakamhifadhi hai yule mtu na jamaa yake yote.
26
Yule mtu akaenda hadi nchi ya Wahiti, ambapo aliujenga mji na kuuita Luzu, ambao ndio jina lake hadi leo.
27
Lakini Manase hawakuwafukuza watu wa Beth-Shani na vijiji vyake, au watu wa Taanaki na vijiji vyake, au watu wa Dori na vijiji vyake, au watu wa Ibleamu na vijiji vyake, au watu wa Megido na vijiji vyake, lakini Wakanaani waliazimu kuishi katika nchi ile.
28
Israeli walipopata nguvu, wakawatia Wakanaani katika kazi ya kulazimishwa, lakini kamwe hawakuwafukuza watoke kabisa.
29
Wala Efraimu hawakuwafukuza kabisa Wakanaani walioishi Gezeri, bali Wakanaani waliendelea kuishi humo miongoni mwao.
30
Vivyo hivyo Zabuloni hawakuwafukuza Wakanaani walioishi huko Kitroni, wala walioishi Nahaloli, ambao walibaki miongoni mwao; bali waliwatia katika kazi ya kulazimishwa.
31
Wala Asheri hawakuwafukuza wale walioishi huko Ako, Sidoni, Alabu, Akzibu, Helba, Afeki wala Rehobu
32
na kwa sababu ya jambo hili Waasheri wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi.
33
Wala Naftali hawakuwafukuza wale walioishi Beth-Shemeshi wala wale walioishi Beth-Anathi; lakini Naftali nao pia wakaishi miongoni mwa Wakanaani, wenyeji wa nchi, nao wale walioishi Beth-Shemeshi na Beth-Anathi wakawa watumishi wao katika kazi ya kulazimishwa.
34
Waamori wakawazuilia Wadani kwenye nchi ya vilima, kwa maana hawakuwaacha washuke kuingia kwenye sehemu tambarare.
35
Waamori pia wakaendelea kukaa katika Mlima Heresi, katika Aiyaloni na Shaalbimu, lakini mkono wa nyumba ya Yosefu ukawalemea, nao wakashindwa hata wakalazimika kuingia katika kazi ya kulazimishwa.
36
Mpaka wa Waamori ulikuwa kuanzia Genge la Akrabimu, kuendelea hadi Sela na kuelekea juu.
Settings