Skip to content
Yohana 5:1-18

Yohana 5:1-18

1
Baada ya haya, kulikuwa na Sikukuu ya Wayahudi, naye Yesu akapanda kwenda Yerusalemu.
2
Huko Yerusalemu, karibu na mlango uitwao Mlango wa Kondoo, palikuwa na bwawa moja lililoitwa kwa Kiebrania Bethzatha, ambalo lilikuwa limezungukwa na kumbi tano.
3
Hapa palikuwa na idadi kubwa ya wasiojiweza, yaani, vipofu, viwete, na waliopooza [wakingojea maji yatibuliwe.
4
Kwa maana malaika alikuwa akishuka wakati fulani, akayatibua maji. Yule aliyekuwa wa kwanza kuingia ndani baada ya maji kutibuliwa alipona ugonjwa wowote aliokuwa nao].
5
Mtu mmoja alikuwako huko ambaye alikuwa ameugua kwa miaka thelathini na minane.
6
Yesu alipomwona akiwa amelala hapo, naye akijua kuwa amekuwa hapo kwa muda mrefu, akamwambia, “Je, wataka kuponywa?”
7
Yule mgonjwa akamjibu, “Bwana, mimi sina mtu wa kuniingiza bwawani maji yanapotibuliwa. Nami ninapotaka kutumbukia bwawani, mtu mwingine huingia kabla yangu.”
8
Yesu akamwambia, “Inuka! Chukua mkeka wako na uende.”
9
Mara yule mtu akapona, akachukua mkeka wake, akaanza kutembea. Basi siku hiyo ilikuwa siku ya Sabato.
10
Kwa hiyo Wayahudi wakamwambia yule mtu aliyeponywa, “Leo ni Sabato, si halali wewe kubeba mkeka wako.”
11
Yeye akawajibu, “Yule mtu aliyeniponya aliniambia, ‘Chukua mkeka wako na uende.’ ”
12
Wakamuuliza, “Ni mtu gani huyo aliyekuambia uchukue mkeka wako uende?”
13
Basi yule mtu aliyeponywa hakufahamu ni nani aliyemponya, kwa sababu Yesu alikuwa amejiondoa katika ule umati wa watu uliokuwa hapo.
14
Baadaye Yesu akamkuta yule mtu aliyemponya ndani ya Hekalu na kumwambia, “Tazama umeponywa, usitende dhambi tena. La sivyo, lisije likakupata jambo baya zaidi.”
15
Yule mtu akaenda, akawaambia wale Wayahudi kuwa ni Yesu aliyemponya.
16
Kwa hiyo Wayahudi wakaanza kumsumbua Yesu, kwa sababu alikuwa anafanya mambo kama hayo siku ya Sabato.
17
Yesu akawajibu, “Baba yangu anafanya kazi yake daima hata siku hii ya leo, nami pia ninafanya kazi.”
18
Maneno haya yaliwaudhi sana viongozi wa Wayahudi. Wakajaribu kila njia wapate jinsi ya kumuua, kwani si kwamba alivunja Sabato tu, bali alikuwa akimwita Mungu Baba yake, hivyo kujifanya sawa na Mungu.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Reading Width 90 chars

Options