Skip to content
Yohana 10:14-38

Yohana 10:14-38

14
“Mimi ndimi mchungaji mwema. Ninawajua kondoo wangu nao kondoo wangu wananijua.
15
Kama vile Baba anavyonijua mimi, nami ninavyomjua Baba, nami nautoa uhai wangu kwa ajili ya kondoo.
16
Ninao kondoo wengine ambao si wa zizi hili, inanipasa kuwaleta, nao wataisikia sauti yangu, hivyo patakuwa na kundi moja na mchungaji mmoja.
17
Baba yangu ananipenda kwa kuwa ninautoa uhai wangu ili niupate tena.
18
Hakuna mtu aniondoleaye uhai wangu, bali ninautoa kwa hiari yangu mwenyewe. Ninao uwezo wa kuutoa uhai wangu na pia ninao uwezo wa kuutwaa tena. Amri hii nimepewa na Baba yangu.”
19
Kwa maneno haya Wayahudi waligawanyika.
20
Wengi wao wakasema, “Huyu amepagawa na pepo mchafu, naye amechanganyikiwa.”
21
Wengine wakasema, “Haya si maneno ya mtu aliyepagawa na pepo mchafu. Je, pepo mchafu aweza kufungua macho ya kipofu?”
22
Wakati huo ilikuwa Sikukuu ya Kuwekwa wakfu kwa Hekalu huko Yerusalemu, nao ulikuwa wakati wa majira ya baridi.
23
Naye Yesu alikuwa akitembea ndani ya Hekalu katika ukumbi wa Solomoni.
24
Wayahudi wakamkusanyikia wakamuuliza, “Utatuweka katika hali ya mashaka mpaka lini? Kama wewe ndiye Kristo tuambie waziwazi.”
25
Yesu akawajibu, “Nimewaambia, lakini hamwamini. Mambo ninayoyatenda kwa jina la Baba yangu yananishuhudia.
26
Lakini hamwamini, kwa sababu ninyi si wa kundi la kondoo wangu.
27
Kondoo wangu huisikia sauti yangu nami nawajua, nao hunifuata,
28
nami ninawapa uzima wa milele, hawataangamia kamwe wala hakuna mtu atakayewapokonya kutoka mikono yangu.
29
Baba yangu aliyenipa hawa ni mkuu kuliko wote na hakuna awezaye kuwapokonya kutoka mikononi mwake.
30
Mimi na Baba yangu tu umoja.”
31
Kwa mara nyingine Wayahudi wakainua mawe ili wampige nayo,
32
lakini Yesu akawaambia, “Nimewaonyesha miujiza mingi mikubwa kutoka kwa Baba yangu. Ni ipi katika hiyo mnataka kunipiga mawe?”
33
Wayahudi wakamjibu, “Hatukupigi mawe kwa sababu ya mambo mema uliyotenda, bali ni kwa kuwa umekufuru. Wewe ingawa ni mwanadamu unajifanya kuwa Mungu.”
34
Yesu akawajibu, “Je, haikuandikwa katika Sheria ya kwamba, ‘Nimesema kuwa, ninyi ni miungu?’
35
Kama aliwaita ‘miungu,’ wale ambao neno la Mungu liliwafikia, nayo Maandiko hayawezi kutanguka,
36
je, mwawezaje kusema kwamba yule ambaye Baba amemweka wakfu na kumtuma ulimwenguni anakufuru, kwa sababu nilisema, ‘Mimi ni Mwana wa Mungu?’
37
Ikiwa sifanyi kazi za Baba yangu, basi msiniamini,
38
lakini ikiwa nazifanya kazi za Mungu, hata kama hamniamini mimi ziaminini hizo kazi, ili mpate kujua na kuelewa kwamba Baba yu ndani yangu, nami ndani yake.”
Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options