Yeremia 33:1-13
1
Wakati Yeremia alipokuwa angali amefungwa kwenye ua wa walinzi, neno la Bwana lilimjia mara ya pili kusema:
2
“Hili ndilo Bwana asemalo, yeye aliyeumba dunia, Bwana aliyeifanya na kuithibitisha, Bwana ndilo jina lake:
3
‘Niite nami nitakuitika na kukuambia mambo makuu na yasiyochunguzika, usiyoyajua.’
4
Kwa maana hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo kuhusu nyumba katika mji huu na majumba ya kifalme ya Yuda yaliyobomolewa ili yatumiwe dhidi ya kule kuzungukwa na jeshi na upanga
5
katika kupigana na Wakaldayo: ‘Zitajazwa na maiti za watu nitakaowachinja katika hasira na ghadhabu yangu. Nitauficha uso wangu kwa sababu ya maovu yake yote.
6
“ ‘Hata hivyo, nitauletea afya na uponyaji, nitawaponya watu wangu na kuwafanya wafurahie amani tele na salama.
7
Nitawarudisha Yuda na Israeli kutoka nchi ya kutekwa kwao, na kuwajenga tena kama walivyokuwa hapo awali.
8
Nitawatakasa dhambi zote walizofanya dhidi yangu, na nitawasamehe dhambi zote za uasi dhidi yangu.
9
Kisha mji huu utaniletea utukufu, furaha, sifa na heshima mbele ya mataifa yote ya dunia yatakayosikia mambo yote mazuri ninayoufanyia. Nao watashangaa na kutetemeka kwa ajili ya wingi wa mafanikio na amani nitakayoupatia.’
10
“Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Mnasema kuhusu mahali hapa kwamba, “Ni mahali palipoachwa ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama.” Lakini katika miji ya Yuda na barabara za Yerusalemu ambazo zimeachwa, ambazo hazikaliwi na wanadamu wala wanyama, huko kutasikika kwa mara nyingine
11
sauti za shangwe na furaha, sauti za bibi na bwana arusi, na sauti za wale waletao sadaka za shukrani katika nyumba ya Bwana, wakisema, “ ‘ “Mshukuruni Bwana Mwenye Nguvu Zote, kwa maana Bwana ni mwema; upendo wake wadumu milele.” Kwa kuwa nitairudishia nchi baraka kama zilivyokuwa hapo awali,’ asema Bwana.
12
“Hili ndilo asemalo Bwana Mwenye Nguvu Zote: ‘Mahali hapa, ambapo ni ukiwa, pasipo na wanadamu wala wanyama: katika miji yake, patakuwepo tena malisho kwa ajili ya wachungaji kupumzisha makundi yao ya kondoo.
13
Katika miji ya nchi ya vilima, ya vilima vya magharibi na ya Negebu, katika nchi ya Benyamini, katika vijiji vinavyoizunguka Yerusalemu na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mkono wa yeye ayahesabuye,’ asema Bwana.
Settings