Yeremia 25:30-38
30
“Basi sasa toa unabii kwa maneno haya yote dhidi yao, uwaambie: “ ‘Bwana atanguruma kutoka juu; atatoa sauti ya ngurumo kutoka makao yake matakatifu na kunguruma kwa nguvu sana dhidi ya nchi yake. Atapiga kelele kama wao wakanyagao zabibu, atapiga kelele dhidi ya wote waishio duniani.
31
Ghasia zitasikika hadi miisho ya dunia, kwa maana Bwana ataleta mashtaka dhidi ya mataifa; ataleta hukumu juu ya wanadamu wote na kuwaua waovu wote,’ ” asema Bwana.
32
Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote asemalo: “Tazama! Maafa yanaenea kutoka taifa moja hadi jingine; tufani kubwa inainuka kutoka miisho ya dunia.”
33
Wakati huo, hao waliouawa na Bwana watatapakaa kila mahali, kuanzia mwisho mmoja wa dunia hadi mwisho mwingine. Hawataombolezewa wala kukusanywa au kuzikwa, lakini watakuwa kama mavi yaliyoenea juu ya ardhi.
34
Lieni na kuomboleza, enyi wachungaji, mgaagae mavumbini, ninyi viongozi wa kundi. Kwa maana wakati wenu wa kuchinjwa umewadia; mtaanguka na kuvunjavunjwa kama vyombo vizuri vya udongo.
35
Wachungaji hawatakuwa na mahali pa kukimbilia, viongozi wa kundi hawatapata mahali pa kutorokea.
36
Sikia kilio cha wachungaji, maombolezo ya viongozi wa kundi, kwa maana Bwana anayaharibu malisho yao.
37
Makao yao ya amani yataharibiwa kwa sababu ya hasira kali ya Bwana.
38
Kama simba ataacha pango lake, nchi yao itakuwa ukiwa kwa sababu ya upanga wa mdhalimu, na kwa sababu ya hasira kali ya Bwana Mungu.
Settings