Mwanzo 37:18-30
18
Ndugu zake walipomwona akiwa mbali, kabla hajawafikia, wakapanga shauri baya la kumuua.
19
Wakaambiana, “Yule mwota ndoto anakuja!
20
Njooni sasa, tumuue na kumtupa katika shimo mojawapo na tuseme kwamba mnyama mkali amemrarua. Kisha tutaona matokeo ya ndoto zake.”
21
Reubeni aliposikia jambo hili, akajaribu kumwokoa kutoka mikononi mwao akasema, “Tusiutoe uhai wake.
22
Tusimwage damu yoyote. Mtupeni katika shimo lililoko hapa jangwani, lakini msimguse.” Reubeni alisema hivyo ili amwokoe kutoka mikononi mwao, kisha amrudishe nyumbani kwa baba yake.
23
Kwa hiyo Yosefu alipowafikia ndugu zake, walimvua lile joho lake, lile joho lililorembwa vizuri alilokuwa amevaa.
24
Kisha wakamchukua wakamtupa katika shimo. Wakati huo shimo lilikuwa tupu, halikuwa na maji ndani yake.
25
Walipokaa ili wale chakula chao, wakainua macho wakaona msafara wa Waishmaeli ukija kutoka Gileadi. Ngamia wao walikuwa wamepakizwa mizigo ya vikolezo, uvumba na manemane, nao walikuwa njiani kuvipeleka Misri.
26
Yuda akawaambia ndugu zake, “Tutafaidi nini ikiwa tutamuua ndugu yetu na kuificha damu yake?
27
Njooni, tumuuze kwa hawa Waishmaeli. Tusimguse, kwa kuwa hata hivyo yeye ni ndugu yetu, nyama yetu na damu yetu wenyewe.” Ndugu zake wakakubali.
28
Kwa hiyo wale wafanyabiashara Wamidiani walipofika pale, ndugu zake wakamtoa Yosefu kutoka kwenye lile shimo, na kumuuza kwa shekeli ishirini za fedha kwa wale Waishmaeli, ambao walimpeleka Misri.
29
Reubeni aliporudi kutazama kwenye lile shimo na kuona kwamba Yosefu hayupo, alirarua nguo zake.
30
Akawarudia ndugu zake na kusema, “Kijana hayuko mle! Nielekee wapi sasa?”
Settings