Ezekieli 16:44-52
44
“ ‘Kila mtu atumiaye maneno ya mithali hii, atayatumia juu yako: “Alivyo mama, ndivyo alivyo bintiye.”
45
Wewe ni binti halisi wa mama yako, ambaye alimchukia kabisa mume wake na watoto wake, tena wewe ni dada halisi wa dada zako, waliowachukia kabisa waume zao na watoto wao. Mama yako alikuwa Mhiti na baba yako alikuwa Mwamori.
46
Dada yako mkubwa alikuwa Samaria, aliyeishi upande wako wa kaskazini na binti zake, pamoja na dada yake, naye dada yako mdogo, aliyeishi kusini yako pamoja na binti zake, alikuwa Sodoma.
47
Hukuziendea njia zao tu na kuiga matendo yao ya kuchukiza, bali kwa muda mfupi katika njia zako zote uliharibika tabia zaidi kuliko wao.
48
Hakika kama niishivyo, asema Bwana Mwenyezi, dada yako Sodoma pamoja na binti zake, kamwe hawakufanya yale ambayo wewe na binti zako mmefanya.
49
“ ‘Sasa hii ilikuwa ndiyo dhambi ya dada yako Sodoma: yeye na binti zake walikuwa na majivuno, walafi na wazembe, hawakuwasaidia maskini na wahitaji.
50
Walijivuna na kufanya mambo ya machukizo sana mbele zangu. Kwa hiyo niliwakatilia mbali nami kama mlivyoona.
51
Samaria hakufanya hata nusu ya dhambi ulizofanya. Wewe umefanya mambo mengi sana ya kuchukiza kuwaliko wao, nawe umewafanya dada zako waonekane kama wenye haki kwa ajili ya mambo haya yote uliyoyafanya.
52
Chukua aibu yako, kwa kuwa umefanya uovu wa dada zako uwe si kitu, nao waonekane kama wenye haki. Kwa kuwa dhambi zako zilikuwa mbaya zaidi kuliko zao, wameonekana wenye haki zaidi kuliko wewe. Kwa hiyo basi, chukua aibu yako, kwa kuwa umewafanya dada zako waonekane wenye haki.
Settings