Kutoka 8:16-28
16
Ndipo Bwana akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyoosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.”
17
Wakafanya hivyo, Aroni aliponyoosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto.
18
Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama.
19
Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile Bwana alivyosema.
20
Kisha Bwana akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi na usimame mbele ya Farao wakati anapokwenda mtoni nawe umwambie, ‘Hili ndilo Bwana asemalo: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu.
21
Kama hutawaachia watu wangu waondoke nitakupelekea makundi ya mainzi juu yako, kwa maafisa wako, kwa watu wako na kwenye nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajazwa mainzi, hata na ardhi yote ya Misri.
22
“ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwepo na makundi ya mainzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, Bwana, niko katika nchi hii.
23
Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ”
24
Naye Bwana akafanya hivyo. Makundi makubwa ya mainzi yalimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na mainzi.
25
Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.”
26
Lakini Mose akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea Bwana Mungu wetu zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Kama tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe?
27
Ni lazima twende mwendo wa siku tatu mpaka tufike jangwani ili tumtolee Bwana Mungu wetu dhabihu, kama alivyotuagiza.”
28
Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea Bwana Mungu wenu dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.”
Settings