Esta 9:1-12
1
Katika siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, yaani mwezi wa Adari, amri iliyoagizwa na mfalme ilikuwa itekelezwe. Siku hii adui wa Wayahudi walikuwa wametumaini kuwashinda, lakini sasa mambo yaliwageukia na Wayahudi wakawashinda wale waliokuwa wanawachukia.
2
Wayahudi walikusanyika katika miji yao, katika majimbo ya Mfalme Ahasuero kuwashambulia wale waliokuwa wanatafuta kuwaangamiza. Hakuna yeyote aliyeweza kushindana nao, kwa sababu watu wa mataifa mengine yote waliwaogopa.
3
Nao wakuu wote wa majimbo, majemadari, watawala na maafisa wa mfalme wakawasaidia Wayahudi, kwa sababu walimhofu Mordekai.
4
Mordekai alikuwa mtu mashuhuri katika jumba la mfalme; sifa zake zilienea katika majimbo yote naye alipata uwezo zaidi na zaidi.
5
Wayahudi waliwaangusha adui zao wote kwa upanga wakiwaua na kuwaangamiza, nao walifanya kile walichotaka kwa wale waliowachukia.
6
Katika ngome ya Shushani Wayahudi waliua na kuangamiza wanaume 500.
7
Pia waliwaua Parshendatha, Dalfoni, Aspatha,
8
Poratha, Adalia, Ardatha,
9
Parmashta, Arisai, Aridai na Waizatha,
10
wana kumi wa Hamani mwana wa Hamedatha, adui wa Wayahudi. Lakini hawakuchukua nyara.
11
Mfalme aliarifiwa siku iyo hiyo hesabu ya waliouawa katika ngome ya Shushani.
12
Mfalme akamwambia Malkia Esta, “Wayahudi wamewaua wanaume 500 na wana kumi wa Hamani ndani ya ngome ya Shushani. Wamefanyaje katika majimbo mengine ya mfalme yaliyobaki? Je, sasa haja yako ni nini? Nayo pia utapewa. Nalo ombi lako ni nini? Nalo utafanyiwa.”
Settings