Danieli 11:5-20
5
“Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi kuliko mfalme, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi.
6
Baada ya miaka kadha, wataungana. Binti wa mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini huyo binti nguvu zake hazitadumu; hata mfalme hatadumu wala nguvu zake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, watoto wake, na yeyote aliyemuunga mkono.
7
“Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake; atapigana dhidi yao naye atashinda.
8
Tena ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma, na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu, na kuvichukua hadi Misri. Kwa miaka kadha atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua.
9
Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia nchi ya mfalme wa Kusini, lakini atarudi nyuma hadi kwenye nchi yake.
10
Wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini.
11
“Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye ataunda jeshi kubwa, lakini litashindwa.
12
Wakati jeshi litakapokuwa limechukuliwa, mfalme wa Kusini atajawa na kiburi na atachinja maelfu mengi, hata hivyo hatabaki na ushindi.
13
Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi jingine kubwa kuliko lile la kwanza; na baada ya miaka kadha, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri.
14
“Katika nyakati hizo wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio.
15
Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzunguka mji kwa majeshi, na kuuteka mji wa ngome. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu za kuyazuia; naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora zaidi, havitakuwa na nguvu ya kuwakabili.
16
Huyo mvamia nchi atafanya apendavyo; hakuna yeyote atakayeweza kumpinga. Atajiimarisha katika Nchi ya Kupendeza, na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza.
17
Ataamua kuja na nguvu za ufalme wake wote na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kuuangusha ufalme, lakini mipango yake haitafanikiwa wala kumsaidia.
18
Ndipo atabadili nia yake kupigana na nchi za pwani na ataziteka nyingi, lakini jemadari mmoja atakomesha ufidhuli wake na kurudisha ufidhuli wake juu yake.
19
Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe, lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.
20
“Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, baada ya miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.
Settings