Matendo 19:1-12
1
Apolo alipokuwa huko Korintho, Paulo alisafiri sehemu za bara, akafika Efeso. Huko akawakuta wanafunzi kadhaa,
2
akawauliza, “Je, mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini?” Wakajibu, “Hapana, hata hatukusikia kuwa kuna Roho Mtakatifu.”
3
Ndipo Paulo akawauliza, “Je, mlibatizwa kwa ubatizo gani?” Wakajibu, “Kwa ubatizo wa Yohana.”
4
Paulo akasema, “Ubatizo wa Yohana ulikuwa wa toba, aliwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja baada yake, yaani, Yesu.”
5
Waliposikia haya, wakabatizwa katika jina la Bwana Yesu.
6
Paulo alipoweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akawashukia, nao wakanena kwa lugha mpya na kutabiri.
7
Walikuwa kama wanaume kumi na wawili.
8
Paulo akaingia katika sinagogi na kunena humo kwa ujasiri kwa muda wa miezi mitatu, akijadiliana na watu na kuwashawishi katika mambo ya Ufalme wa Mungu.
9
Lakini baadhi yao walikaidi. Walikataa kuamini, na wakakashifu ujumbe wake mbele ya umati wa watu. Basi Paulo aliachana nao. Akawachukua wanafunzi naye, akahojiana nao kila siku katika darasa la Tirano.
10
Jambo hili likaendelea kwa muda wa miaka miwili, kiasi kwamba Wayahudi na Wayunani wote walioishi huko Asia wakawa wamesikia neno la Bwana.
11
Mungu akafanya miujiza mingi isiyo ya kawaida kwa mkono wa Paulo,
12
hivi kwamba leso au vitambaa vilivyokuwa vimegusa mwili wa Paulo viliwekwa juu ya wagonjwa, nao wakapona magonjwa yao, na pepo wachafu wakawatoka.
Settings