2 Nyakati 36:11-21
11
Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala, naye akatawala huko Yerusalemu kwa miaka kumi na mmoja.
12
Alifanya maovu machoni pa Bwana Mungu wake, wala hakujinyenyekeza mbele ya nabii Yeremia, ambaye alinena neno la Bwana.
13
Pia alimwasi Mfalme Nebukadneza, ambaye alikuwa amemwapisha kwa jina la Mungu. Akashupaza shingo na akafanya moyo wake kuwa mgumu wala hakutaka kumgeukia Bwana, Mungu wa Israeli.
14
Zaidi ya hayo viongozi wote wa makuhani pamoja na watu wakazidi kukosa uaminifu zaidi na zaidi, wakafanya machukizo yote kama walivyofanya mataifa wakinajisi Hekalu la Bwana alilokuwa amelitakasa huko Yerusalemu.
15
Bwana, Mungu wa baba zao, akawapelekea neno kupitia wajumbe wake tena na tena, kwa sababu alikuwa anawahurumia watu wake pamoja na mahali pa maskani yake.
16
Lakini waliwadhihaki wajumbe wa Bwana wakayadharau maneno yake na kuwacheka manabii wake mpaka ghadhabu ya Bwana ikawa kubwa dhidi ya watu wake na hakukuwa na namna ya kuituliza.
17
Mungu akamwinua dhidi yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao wa kiume kwa upanga ndani ya mahali patakatifu, ambaye hakumbakiza kijana mwanaume wala kijana mwanamke, wazee wala vikongwe. Mungu akawatia wote mikononi mwa Nebukadneza.
18
Akavichukua kwenda Babeli vyombo vyote kutoka Hekalu la Mungu, vikubwa na vidogo, hazina za Hekalu la Bwana pamoja na hazina za mfalme na za maafisa wake.
19
Wakalichoma Hekalu la Mungu na kuzibomoa kuta za Yerusalemu, wakachoma moto majumba yote ya kifalme na kuharibu kila kitu chake cha thamani.
20
Wale watu walionusurika kuuawa kwa upanga wakachukuliwa kwenda uhamishoni Babeli. Nao wakawa watumishi wake na wa wanawe mpaka wakati wa utawala wa ufalme wa Uajemi ulifika.
21
Nchi ikaendelea kufurahia pumziko lake la Sabato, wakati wote wa kufanywa kwake ukiwa ilipumzika mpaka ile miaka sabini ilipotimia katika kutimiza neno la Bwana lililonenwa na Yeremia.
Settings