Skip to content
2 Nyakati 32:1-8

2 Nyakati 32:1-8

1
Baada ya yale yote aliyokuwa amefanya Hezekia kwa uaminifu mkubwa, Senakeribu mfalme wa Ashuru akaja na kuvamia Yuda. Akaizunguka miji yenye ngome kwa jeshi, akifikiri kuiteka iwe yake.
2
Hezekia alipoona kuwa Senakeribu amekuja na kwamba alikusudia kufanya vita juu ya Yerusalemu,
3
akafanya shauri na maafisa wake na mashujaa wake juu ya kuzuia maji kutoka chemchemi zilizo nje ya mji, nao wakamsaidia.
4
Umati mkubwa wa watu ukakusanyika na kuzuia chemchemi zote na vijito vilivyotiririka katika nchi yote, wakisema: “Kwa nini wafalme wa Ashuru waje na kukuta maji tele?”
5
Hezekia akafanya kazi kwa bidii kukarabati sehemu zote zilizokuwa zimebomoka za ukuta na kujenga minara juu yake. Akajenga ukuta mwingine nje ya ule uliokuwepo na kuimarisha Milo katika Mji wa Daudi. Akatengeneza pia silaha nyingi na ngao.
6
Akaweka maafisa wa jeshi juu ya watu, wakawakutanisha mbele yake katika uwanja kwenye lango la mji, naye akawatia moyo kwa maneno haya:
7
“Kuweni hodari na wenye moyo mkuu. Msiogope, msifadhaike wala msikate tamaa kwa sababu ya mfalme wa Ashuru na hili jeshi kubwa lililo pamoja naye, kwa kuwa aliye pamoja nasi ni mkuu kuliko aliye pamoja naye.
8
Kwake uko mkono wa mwili tu, bali kwetu yuko Bwana Mungu wetu kutusaidia na kutupigania vita vyetu.” Nao watu wakatiwa moyo kutokana na maneno aliyowaambia Hezekia mfalme wa Yuda.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options