1 Samweli 17:12-30
12
Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefrathi jina lake Yese aliyekuwa ametoka Bethlehemu ya Yuda. Yese alikuwa na wana wanane, naye wakati wa Sauli alikuwa mzee tena wa umri mkubwa.
13
Wana wakubwa watatu wa Yese walikuwa wamefuatana na Sauli vitani: Mzaliwa wa kwanza alikuwa Eliabu, wa pili Abinadabu, na wa tatu Shama.
14
Daudi ndiye alikuwa mdogo wa wote. Hao wakubwa watatu wakamfuata Sauli,
15
lakini Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili kuchunga kondoo wa baba yake huko Bethlehemu.
16
Kwa siku arobaini huyo Mfilisti alikuwa akija mbele kila siku asubuhi na jioni na kujionyesha.
17
Wakati huo Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Chukua hii efa ya bisi na hii mikate kumi kwa ajili ya ndugu zako uwapelekee upesi kambini mwao.
18
Chukua pamoja na hizi jibini kumi kwa jemadari wa kikosi chao. Ujue hali ya ndugu zako na uniletee taarifa za uhakika kutoka kwao.
19
Wao wako pamoja na Sauli na watu wote wa Israeli huko kwenye Bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.”
20
Asubuhi na mapema Daudi akaondoka, akaliacha kundi la kondoo pamoja na mchungaji, akapakia vitu vile na kuondoka, kama vile Yese alivyokuwa amemwagiza. Akafika kambini wakati jeshi lilikuwa likitoka kwenda kwenye sehemu yake ya kupigania, huku wakipiga kelele za vita.
21
Israeli na Wafilisti walikuwa wakipanga safu zao wakitazamana.
22
Daudi akaacha vile vitu vyake kwa mtunza vifaa, akakimbilia katika safu za vita na kuwasalimu ndugu zake.
23
Alipokuwa akisema nao, Goliathi, yule Mfilisti shujaa kutoka Gathi, akajitokeza mbele ya safu zake na kupiga ile kelele yake ya kawaida ya matukano, naye Daudi akayasikia.
24
Waisraeli walipomwona yule mtu, wote wakamkimbia kwa woga mkuu.
25
Basi Waisraeli walikuwa wakisema, “Je, mnaona jinsi mtu huyu anavyoendelea kujitokeza. Hujitokeza ili kutukana Israeli. Mfalme atatoa utajiri mwingi kwa yule mtu atakayemuua. Pia atamwoza binti yake na atasamehe jamaa ya baba yake kulipa kodi katika Israeli.”
26
Daudi akauliza watu waliokuwa wamesimama karibu naye, “Je, atafanyiwa nini mtu atakayemuua huyu Mfilisti na kuondoa aibu hii katika Israeli? Ni nani huyu Mfilisti asiyetahiriwa hata atukane majeshi ya Mungu aliye hai?”
27
Wakarudia yale yaliyokuwa yamesemwa na kumwambia kuwa, “Hili ndilo atakalotendewa mtu yule atakayemuua.”
28
Eliabu nduguye mkubwa Daudi alipomsikia akizungumza na watu hasira ikawaka juu yake akamuuliza, “Kwa nini umeteremka kuja hapa? Nao wale kondoo wachache kule nyikani umewaacha na nani? Ninajua jinsi ulivyo na kiburi na jinsi moyo wako ulivyo mwovu; umekuja hapa kutazama vita tu.”
29
Daudi akasema, “Sasa nimefanya nini? Je, siwezi hata kuongea.”
30
Daudi akamgeukia mtu mwingine na kumuuliza jambo lilo hilo, nao watu wakamjibu vilevile kama mwanzo.
Settings