1 Wafalme 4:20-34
20
Watu wa Yuda na Israeli walikuwa wengi kama mchanga wa pwani; walikula, wakanywa na kufurahi.
21
Mfalme Solomoni akatawala katika falme zote kuanzia Mto Frati hadi nchi ya Wafilisti, hadi kwenye mpaka wa Misri. Nchi hizi zilileta ushuru na zilikuwa chini ya Solomoni, siku zote za maisha yake.
22
Mahitaji ya Solomoni ya kila siku yalikuwa kori thelathini za unga laini, kori sitini za unga wa kawaida.
23
Ngʼombe kumi wa zizini, ngʼombe ishirini wa malisho, kondoo na mbuzi mia moja, pamoja na ayala, paa, kulungu na kuku wazuri sana.
24
Kwa kuwa Solomoni alitawala falme zote magharibi ya mto, kuanzia Tifsa hadi Gaza, naye akawa na amani pande zote.
25
Wakati wa maisha ya Solomoni Yuda na Israeli, kuanzia Dani mpaka Beer-Sheba, wakaishi salama kila mtu chini ya mzabibu wake na chini ya mtini wake.
26
Solomoni alikuwa na mabanda 4,000 ya magari ya vita, na farasi 12,000.
27
Maafisa wa eneo hilo, kila mmoja katika mwezi wake, walileta mahitaji kwa ajili ya Mfalme Solomoni na wote waliokula mezani mwa mfalme. Walihakikisha kuwa hakuna chochote kilichopungua.
28
Pia walileta sehemu walizopangiwa za shayiri na majani kwa ajili ya farasi wavutao magari na farasi wengine mahali palipostahili.
29
Mungu akampa Solomoni hekima na akili kubwa, pia ufahamu mpana usiopimika kama mchanga ulioko pwani ya bahari.
30
Hekima ya Solomoni ilikuwa kubwa kuliko hekima ya watu wote wa Mashariki na kubwa kuliko hekima yote ya Misri.
31
Alikuwa na hekima kuliko kila mwandishi, akiwemo Ethani Mwezrahi: kuliko Hemani, Kalkoli na Darda, wana wa Maholi. Umaarufu wake ukaenea kwa mataifa yote yaliyomzunguka.
32
Akanena mithali 3,000 na nyimbo zake zilikuwa 1,005.
33
Akaelezea maisha ya mimea kuanzia mwerezi wa Lebanoni hadi hisopo iotayo ukutani. Pia akafundisha kuhusu wanyama na ndege, wanyama wenye damu baridi, wakiwemo samaki.
34
Watu wa mataifa yote wakaja kusikiliza hekima ya Solomoni, waliotumwa na wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamesikia juu ya hekima yake.
Settings