Ufunuo 18:2-8
2
Naye akalia kwa nguvu kwa sauti kubwa, akisema: “Umeanguka! Umeanguka Babeli Mkuu! Umekuwa makao ya mashetani na makazi ya kila pepo mchafu, makazi ya kila ndege na kila mnyama achukizaye.
3
Kwa maana mataifa yote yamekunywa mvinyo wa ghadhabu ya uasherati wake. Nao wafalme wa dunia wamefanya uzinzi nao, nao wafanyabiashara wa dunia wametajirika kutokana na wingi wa utajiri wake.”
4
Kisha nikasikia sauti nyingine kutoka mbinguni ikisema: “Tokeni katikati yake, enyi watu wangu, ili msije mkashiriki dhambi zake, ili msije mkapatwa na pigo lake lolote;
5
kwa kuwa dhambi zake zimelundikana hadi mbinguni, naye Mungu ameukumbuka uhalifu wake.
6
Mtendee kama yeye alivyotenda; umlipe mara mbili kwa ajili ya yale aliyotenda. Katika kikombe chake mchanganyie mara mbili ya kile alichochanganya.
7
Mpatie mateso na huzuni nyingi sawa na utukufu na anasa alizojipatia. Kwa kuwa moyoni mwake hujivuna, akisema, ‘Mimi ninatawala kama malkia; mimi si mjane, wala sitaona huzuni kamwe.’
8
Kwa hiyo mapigo yatampata kwa siku moja: mauti, maombolezo na njaa. Naye atateketezwa kwa moto, kwa maana Bwana Mungu amhukumuye ana nguvu.
Settings