Mathayo 21:1-9
1
Walipokaribia Yerusalemu, wakafika Bethfage katika Mlima wa Mizeituni. Ndipo Yesu akawatuma wanafunzi wake wawili,
2
akawaambia, “Nendeni katika kijiji kilichoko mbele yenu, nanyi mtamkuta punda amefungwa hapo, na mwana-punda pamoja naye. Wafungueni na mniletee.
3
Kama mtu yeyote akiwasemesha lolote, mwambieni kwamba Bwana ana haja nao, naye atawaruhusu mwalete mara.”
4
Haya yalitukia ili litimie lile lililonenwa na nabii, akisema:
5
“Mwambieni Binti Sayuni, ‘Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mnyenyekevu, naye amepanda punda, juu ya mwana-punda, mtoto wa punda.’ ”
6
Wale wanafunzi wakaenda, wakafanya kama Yesu alivyokuwa amewaagiza.
7
Wakamleta yule punda na mwana-punda, nao wakatandika mavazi yao juu ya hao punda, naye Yesu akaketi juu yake.
8
Umati mkubwa wa watu ukatandaza mavazi yao barabarani, na wengine wakakata matawi kutoka kwenye miti, wakayatandaza barabarani.
9
Ule umati wa watu uliomtangulia na ule uliomfuata ukapiga kelele ukisema, “Hosana, Mwana wa Daudi!” “Amebarikiwa yeye ajaye kwa Jina la Bwana!” “Hosana juu mbinguni!”
Settings