Luka 10:1-11
1
Baada ya hayo, Bwana akawachagua wengine sabini na wawili, akawatuma wawili wawili katika kila mji na kila sehemu aliyokusudia kwenda baadaye.
2
Akawaambia, “Mavuno ni mengi, lakini watendakazi ni wachache. Kwa hiyo mwombeni Bwana wa mavuno, ili apeleke watendakazi katika shamba lake la mavuno.
3
Haya! nendeni. Ninawatuma kama wana-kondoo katikati ya mbwa mwitu.
4
Msichukue mkoba, wala mfuko, wala viatu, na msimsalimu mtu yeyote njiani.
5
“Mkiingia katika nyumba yoyote, kwanza semeni, ‘Amani iwe kwenu.’
6
Kama kuna mtu wa amani humo, basi amani yenu itakuwa juu yake. La sivyo, itawarudia.
7
Kaeni katika nyumba hiyo, mkila na kunywa kile watakachowapa, kwa sababu kila mtendakazi anastahili malipo yake. Msihamehame kutoka nyumba hadi nyumba.
8
“Mkienda katika mji na watu wake wakawakaribisha, kuleni chochote kiwekwacho mbele yenu,
9
waponyeni wagonjwa waliomo na waambieni: ‘Ufalme wa Mungu umekaribia.’
10
Lakini mkiingia katika mji, nao hawakuwakaribisha, tokeni mwende katika barabara zake mkaseme:
11
‘Hata mavumbi ya mji wenu yaliyoshikamana na miguu yetu, tunayakungʼuta dhidi yenu. Lakini mjue kwamba Ufalme wa Mungu umekaribia.’
Settings