Walawi 14:33-53
33
Bwana akawaambia Mose na Aroni,
34
“Mtakapoingia katika nchi ya Kanaani ambayo ninawapa kuwa milki yenu, nami nikaweka upele ueneao kwenye nyumba katika nchi ile,
35
ni lazima mwenye nyumba hiyo akamwambie kuhani, ‘Nimeona kitu fulani kinachofanana na upele kwenye nyumba yangu.’
36
Kuhani ataagiza vitu vyote vitolewe ndani ya nyumba, kabla hajaenda kuchunguza kama ina ugonjwa huo, ili kitu chochote ndani ya nyumba kisitangazwe kuwa najisi. Baada ya hili, kuhani ataingia ndani na kuikagua hiyo nyumba.
37
Atachunguza upele huo katika kuta za nyumba hiyo, nazo kama zina rangi ya kijani kibichi au wekundu, na kuna mibonyeo ndani ya ukuta,
38
kuhani atatoka na kufunga mlango wa nyumba hiyo kwa siku saba.
39
Siku ya saba, kuhani atarudi kuikagua nyumba. Kama upele umeenea juu ya kuta,
40
ataagiza kwamba mawe yote yaliyoambukizwa yaondolewe na kutupwa katika eneo lililo najisi nje ya mji.
41
Kuta zote za ndani ya nyumba hiyo ni lazima zikwanguliwe, na kifusi chake kitupwe mahali najisi nje ya mji.
42
Kisha watachukua mawe mengine na kujenga palipobomolewa kwa udongo mpya wa mfinyanzi, na kuipiga nyumba hiyo lipu mpya.
43
“Ikiwa upele huo utatokea tena ndani ya ile nyumba baada ya mawe kuondolewa na nyumba kukwanguliwa na kuwekwa lipu mpya,
44
kuhani atakwenda kuikagua, na kama upele umeenea ndani ya nyumba, basi ni upele uharibuo; nyumba hiyo ni najisi.
45
Ni lazima ibomolewe: mawe yake, mbao na lipu yake, vyote vikatupwe nje ya mji mahali palipo najisi.
46
“Yeyote atakayeingia katika nyumba hiyo ikiwa imefungwa, atakuwa najisi mpaka jioni.
47
Yeyote atakayelala au kula ndani ya nyumba hiyo ni lazima afue nguo zake.
48
“Lakini ikiwa kuhani atakuja kuikagua na kukuta kuwa upele haujaenea tena baada ya nyumba kupigwa lipu, ataitangaza nyumba ile kuwa safi, kwa sababu upele umekwisha.
49
Ili kuitakasa nyumba hiyo, mwenye nyumba ataleta ndege wawili, mti wa mwerezi, kitani nyekundu na hisopo.
50
Atamchinja mmoja wa wale ndege kwenye chungu chenye maji safi.
51
Kisha atachukua mti wa mwerezi, hisopo, kitani nyekundu na ndege aliye hai, na kuvitumbukiza ndani ya damu ya ndege aliyechinjwa pamoja na maji safi, na kuinyunyizia nyumba ile mara saba.
52
Ataitakasa nyumba kwa damu ya yule ndege, maji safi, ndege aliye hai, mti wa mwerezi, hisopo na kitani nyekundu.
53
Kisha atamwachia yule ndege aliye hai huru mashambani nje ya mji. Kwa njia hii atafanya upatanisho kwa ajili ya nyumba ile, nayo itakuwa safi.”
Settings