Waamuzi 6:8-30
8
Bwana akawapelekea nabii, ambaye aliwaambia, “Hili ndilo Bwana, Mungu wa Israeli, asemalo: Niliwapandisha mtoke Misri, toka nchi ya utumwa.
9
Nikawanyakua kutoka mikononi mwa Wamisri na kutoka mikononi mwa watesi wenu wote. Nikawafukuza watoke mbele yenu nami nikawapa ninyi nchi yao.
10
Nikawaambia, ‘Mimi ndimi Bwana Mungu wenu; msiiabudu miungu ya Waamori, ambayo mnakaa katika nchi yao!’ Lakini ninyi hamkuitii sauti yangu.”
11
Malaika wa Bwana akaja akaketi chini ya mti wa mwaloni huko Ofra, ambao ulikuwa mali ya Yoashi, Mwabiezeri, ambako Gideoni mwanawe alikuwa akipepeta ngano penye shinikizo la kukamulia zabibu, ili kuificha Wamidiani wasiione.
12
Malaika wa Bwana alipomtokea Gideoni, akamwambia, “Bwana yu pamoja nawe, Ewe shujaa mwenye nguvu.”
13
Gideoni akajibu, “Ee Bwana wangu, kama Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametutokea? Yako wapi basi yale matendo yake makuu baba zetu waliyotusimulia juu yake waliposema, ‘Je, Bwana hakutupandisha kutoka Misri?’ Lakini sasa Bwana ametuacha na kututia katika mkono wa Midiani.”
14
Bwana akamgeukia na kusema “Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli kutoka mikononi mwa Wamidiani. Je, si mimi ninayekutuma wewe?”
15
Gideoni akauliza, “Ee Bwana wangu, nitawezaje kuwaokoa Israeli? Ukoo wangu ndio dhaifu kuliko zote katika Manase, nami ndiye mdogo wa wote katika jamaa yangu.”
16
Bwana akamjibu, “Nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kana kwamba walikuwa ni mtu mmoja.”
17
Gideoni akajibu, “Kama basi nimepata kibali machoni pako, nipe ishara kuonyesha kweli kwamba ni wewe unayesema nami.
18
Tafadhali ninakuomba usiondoke hapa mpaka nitakaporudi na kukuletea sadaka yangu na kuiweka mbele yako.” Naye Bwana akamwambia, “Nitangoja mpaka utakaporudi.”
19
Gideoni akaingia ndani ya nyumba yake na kuandaa mwana-mbuzi pamoja na kuoka mikate isiyotiwa chachu kutokana na efa moja ya unga. Akaweka nyama kwenye kikapu na mchuzi kwenye chungu, akamletea huyo malaika hapo nje chini ya mti wa mwaloni na kumpa.
20
Malaika wa Mungu akamwambia, “Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uviweke juu ya mwamba huu na umimine huo mchuzi juu yake.” Gideoni akafanya hivyo.
21
Malaika wa Bwana akainyoosha fimbo iliyokuwa mkononi mwake, ncha yake ikagusa ile nyama na ile mikate isiyotiwa chachu, nao moto ukatoka kwenye mwamba ukateketeza ile nyama na ile mikate. Malaika wa Bwana akatoweka kutoka machoni pake.
22
Gideoni alipotambua kuwa ni malaika wa Bwana, akapiga kelele kwa mshangao, akasema, “Ole wangu, Bwana Mwenyezi! Kwa kuwa nimemwona malaika wa Bwana uso kwa uso!”
23
Lakini Bwana akamwambia, “Amani iwe kwako! Usiogope. Hutakufa.”
24
Hivyo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu mahali pale na kupaita, Yehova-Shalom. Mpaka leo ingalipo imesimama huko Ofra ya Waabiezeri.
25
Usiku ule ule Bwana akamwambia, “Mchukue ngʼombe dume wa baba yako, yaani, yule wa pili mwenye miaka saba, na ubomoe madhabahu ya Baali aliyo nayo baba yako, na ukaikate Ashera iliyo karibu nayo.
26
Kisha mjengee Bwana Mungu wako, madhabahu halisi, kwa taratibu zake, juu ya huu mwamba. Kwa kutumia kuni za hiyo nguzo ya Ashera uliyoikatakata, mtoe sadaka huyo dume wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa.”
27
Basi Gideoni akawachukua watumishi wake kumi na kufanya kama Bwana alivyomwambia. Lakini kwa kuwa aliwaogopa jamaa yake na watu wa mji, akafanya haya usiku badala ya mchana.
28
Watu wa mji walipoamka asubuhi, tazama madhabahu ya Baali imebomolewa na nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwakatwa na yule ngʼombe wa pili ametolewa sadaka juu ya madhabahu yaliyojengwa upya!
29
Wakaulizana, “Ni nani aliyetenda mambo haya?” Walipochunguza kwa makini, wakaambiwa, “Ni Gideoni mwana wa Yoashi, ndiye alitenda hivi.”
30
Watu wa mji wakamwambia Yoashi, “Mlete mwanao hapa. Ni lazima afe, kwa sababu amebomoa madhabahu ya Baali na kukatakata nguzo ya Ashera iliyokuwa karibu nayo.”
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings