Yoshua 9:15-27
15
Ndipo Yoshua akafanya mapatano ya amani pamoja nao kuwaacha waishi, nao viongozi wa kusanyiko wakathibitisha kwa kiapo.
16
Siku ya tatu baada ya hao kufanya mapatano na Wagibeoni, Waisraeli wakapata habari kuwa hao watu ni jirani zao waliokuwa wanaishi karibu nao.
17
Ndipo wana wa Israeli wakasafiri na siku ya tatu wakafika kwenye miji yao ya Gibeoni, Kefira, Beerothi na Kiriath-Yearimu.
18
Lakini Waisraeli hawakuwashambulia kwa kuwa viongozi wa kusanyiko walikuwa wamewaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli. Kusanyiko lote likanungʼunika dhidi ya hao viongozi,
19
lakini viongozi wote wakawajibu, “Tumeshawaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli, kwa hiyo hatuwezi kuwagusa sasa.
20
Hivi ndivyo tutakavyowafanyia: Tutawaacha waishi, ili ghadhabu isije juu yetu kwa kuvunja kiapo tulichowaapia.”
21
Wakaendelea kusema, “Waacheni waishi, lakini wawe wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii yote.” Hivyo ahadi waliyoweka viongozi kwao ikawa hivyo.
22
Kisha Yoshua akawaita Wagibeoni na kuwaambia, “Kwa nini mmetudanganya kwa kutuambia, ‘Tunaishi mbali nanyi,’ wakati ambapo ninyi mnaishi karibu nasi?
23
Sasa mko chini ya laana: Daima mtakuwa wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.”
24
Wakamjibu Yoshua, “Watumwa wako waliambiwa waziwazi jinsi Bwana Mungu wenu alivyomwamuru mtumishi wake Mose kuwapa ninyi nchi hii yote na kuwaangamiza wakazi wake wote toka mbele zenu. Kwa hiyo tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, ndiyo maana tukafanya neno hili.
25
Sasa tupo mikononi mwako. Tufanyieni lolote mnaloona kuwa jema na haki kwako.”
26
Kwa hiyo Yoshua akawaokoa mikononi mwa Waisraeli, nao hawakuuawa.
27
Siku hiyo Yoshua akawafanya Wagibeoni wapasua kuni na wachota maji kwa ajili ya jamii na kwa ajili ya madhabahu ya Bwana mahali pale ambapo Bwana angepachagua. Hivyo ndivyo walivyo hadi hivi leo.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings