Yohana 7:32-49
32
Mafarisayo wakasikia watu wakinongʼona mambo kama hayo kuhusu Yesu, ndipo wao pamoja na viongozi wa makuhani wakatuma walinzi wa Hekalu waende kumkamata.
33
Yesu akasema, “Mimi bado niko pamoja nanyi kwa kitambo kidogo, kisha nitarudi kwake yeye aliyenituma.
34
Mtanitafuta lakini hamtaniona, nami niliko ninyi hamwezi kuja.”
35
Wayahudi wakaulizana wao kwa wao, “Huyu mtu anataka kwenda wapi ambako hatuwezi kumfuata? Je, anataka kwenda kwa Wayunani ambako baadhi ya watu wetu wametawanyikia, akawafundishe Wayunani?
36
Yeye ana maana gani anaposema, ‘Mtanitafuta lakini hamtaniona,’ na, ‘nami niliko ninyi hamwezi kuja’?”
37
Siku ile ya mwisho ya Sikukuu, siku ile kuu, wakati Yesu akiwa amesimama huko, akapaza sauti yake akasema, “Kama mtu yeyote anaona kiu na aje kwangu anywe.
38
Yeyote aniaminiye mimi, kama Maandiko yasemavyo, vijito vya maji ya uzima vitatiririka ndani mwake.”
39
Yesu aliposema haya alimaanisha Roho Mtakatifu ambaye wote waliomwamini wangempokea, kwani mpaka wakati huo, Roho alikuwa hajatolewa, kwa kuwa Yesu alikuwa bado hajatukuzwa.
40
Waliposikia maneno hayo, baadhi ya watu miongoni mwa ule umati wakasema, “Hakika huyu ndiye yule Nabii.”
41
Wengine wakasema, “Huyu ndiye Kristo!” Lakini wengine wakauliza, “Je, Kristo kwao ni Galilaya?
42
Je, Maandiko hayasemi kwamba Kristo atakuja kutoka jamaa ya Daudi na kutoka Bethlehemu, mji alioishi Daudi?”
43
Kwa hiyo watu wakagawanyika kwa ajili ya Yesu.
44
Baadhi yao walitaka kumkamata, lakini hakuna aliyethubutu kumgusa.
45
Hatimaye wale walinzi wa Hekalu wakarudi kwa viongozi wa makuhani na Mafarisayo waliokuwa wamewatuma ili kumkamata Yesu, wakaulizwa, “Mbona hamkumkamata?”
46
Wale walinzi wakajibu, “Kamwe hajanena mtu yeyote kama yeye anenavyo.”
47
Mafarisayo wakajibu, “Je, nanyi pia mmedanganyika?
48
Je, kuna kiongozi yeyote au mmoja wa Mafarisayo ambaye amemwamini?
49
Lakini huu umati wa watu wasiojua Sheria ya Mose, wamelaaniwa.”
Settings