Yoeli 2:18-32
18
Kisha Bwana atakuwa na wivu kwa ajili ya nchi yake na kuwa na huruma juu ya watu wake.
19
Bwana atawajibu: “Ninawapelekea nafaka, mvinyo mpya na mafuta, vya kuwatosha ninyi hadi mridhike kabisa; kamwe sitawafanya tena kitu cha kudharauliwa na mataifa.
20
“Nitafukuza jeshi la kaskazini likae mbali nanyi, nikilisukuma ndani ya jangwa, askari wa safu za mbele wakienda ndani ya bahari ya mashariki na wale wa safu za nyuma katika bahari ya magharibi. Uvundo wake utapaa juu; harufu yake itapanda juu.” Hakika ametenda mambo makubwa.
21
Usiogope, ee nchi; furahi na kushangilia. Hakika Bwana ametenda mambo makubwa.
22
Msiogope, enyi wanyama pori, kwa kuwa mbuga za malisho yenu zinarudia ubichi. Miti nayo inazaa matunda, mtini na mzabibu inatoa utajiri wake.
23
Furahini, enyi watu wa Sayuni, shangilieni katika Bwana Mungu wenu, kwa kuwa amewapa mvua za vuli kwa kipimo cha haki. Anawapelekea mvua nyingi, mvua ya vuli na ya masika, kama mwanzoni.
24
Sakafu za kupuria zitajaa nafaka, mapipa yatafurika mvinyo mpya na mafuta.
25
“Nitawalipa kwa ajili ya miaka ile iliyoliwa na nzige: parare, madumadu na tunutu, jeshi langu kubwa ambalo nililituma katikati yenu.
26
Mtakuwa na wingi wa vyakula mpaka mshibe, na mtalisifu jina la Bwana Mungu wenu, ambaye amefanya maajabu kwa ajili yenu; kamwe watu wangu hawataaibishwa tena.
27
Ndipo mtakapojua kwamba mimi niko katika Israeli kwamba mimi ndimi Bwana Mungu wenu, na kwamba hakuna mwingine; kamwe watu wangu hawataaibika tena.
28
“Hata itakuwa, baada ya hayo, nitamimina Roho wangu juu ya wote wenye mwili. Wana wenu na binti zenu watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono.
29
Hata juu ya watumishi wangu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile nitamimina Roho wangu.
30
Nami nitaonyesha maajabu katika mbingu na duniani: damu, moto na mawimbi ya moshi.
31
Jua litageuzwa kuwa giza na mwezi kuwa mwekundu kama damu, kabla ya kuja siku ya Bwana ile kuu na ya kutisha.
32
Na kila mtu atakayeliitia jina la Bwana ataokolewa. Kwa maana juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu kutakuwepo wokovu, kama Bwana alivyosema, miongoni mwa walionusurika ambao Bwana awaita.
Settings