Yeremia 30:1-12
1
Hili ndilo neno lililomjia Yeremia kutoka kwa Bwana:
2
“Hili ndilo asemalo Bwana, Mungu wa Israeli: ‘Andika katika kitabu maneno yote niliyonena na wewe.
3
Siku zinakuja,’ asema Bwana, ‘nitakapowaleta watu wangu Israeli na Yuda kutoka uhamishoni, na kuwarudisha katika nchi niliyowapa baba zao ili kuimiliki,’ asema Bwana.”
4
Haya ndiyo maneno Bwana aliyoyanena kuhusu Israeli na Yuda:
5
“Hili ndilo asemalo Bwana: “ ‘Vilio vya woga vinasikika: hofu kuu, wala si amani.
6
Ulizeni na mkaone: Je, mwanaume aweza kuzaa watoto? Kwa nini basi ninaona kila mwanaume mwenye nguvu ameweka mikono yake tumboni kama mwanamke aliye na utungu wa kuzaa, kila uso ukigeuka rangi kabisa?
7
Tazama jinsi ile siku itakavyokuwa ya kutisha! Hakutakuwa na nyingine mfano wake. Utakuwa wakati wa dhiki kwa Yakobo, lakini ataokolewa kutoka hiyo.
8
“ ‘Katika siku ile,’ asema Bwana Mwenye Nguvu Zote, ‘nitaivunja nira kutoka shingoni mwao na kuvipasua vifungo vyao; wageni hawatawafanya tena watumwa.
9
Badala yake, watamtumikia Bwana, Mungu wao na Daudi mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.
10
“ ‘Hivyo usiogope, ee Yakobo mtumishi wangu, usifadhaike, ee Israeli,’ asema Bwana. ‘Hakika, nitakuokoa kutoka mbali, wazao wako kutoka nchi ya uhamisho wao. Yakobo atakuwa tena na amani na usalama, wala hakuna atakayemtia hofu.
11
Mimi niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,’ asema Bwana. ‘Ingawa nitayaangamiza kabisa mataifa yote ambamo miongoni mwao nimewatawanya, sitawaangamiza ninyi kabisa. Nitawaadhibu, lakini kwa haki. Sitawaacha kabisa bila adhabu.’
12
“Hili ndilo asemalo Bwana: “ ‘Kidonda chako hakina dawa, jeraha lako haliponyeki.
Settings