Yeremia 28:1-11
1
Katika mwezi wa tano wa mwaka ule ule, yaani mwaka wa nne, mwanzoni mwa utawala wa Sedekia mfalme wa Yuda, nabii Hanania mwana wa Azuri, ambaye alitoka Gibeoni, akaniambia katika nyumba ya Bwana mbele ya makuhani na watu wote:
2
“Hili ndilo Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wa Israeli asemalo: ‘Nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.
3
Katika muda wa miaka miwili nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya Bwana ambavyo Nebukadneza mfalme wa Babeli aliviondoa kutoka hapa na kuvipeleka Babeli.
4
Pia nitamrudisha mahali hapa Yekonia mwana wa Yehoyakimu mfalme wa Yuda, pamoja na wote waliohamishwa kutoka Yuda ambao walikwenda Babeli,’ asema Bwana, ‘kwa kuwa nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.’ ”
5
Ndipo nabii Yeremia akamjibu nabii Hanania mbele ya makuhani na watu wote waliokuwa wamesimama ndani ya nyumba ya Bwana.
6
Akasema, “Amen! Bwana na afanye hivyo! Bwana na ayatimize maneno uliyotoa unabii kwa kuvirudisha mahali hapa kutoka Babeli vyombo vya nyumba ya Bwana pamoja na wote waliohamishwa.
7
Hata hivyo, nisikilize nikuambie yale nitakayoyasema masikioni mwako na masikioni mwa watu hawa wote:
8
Tangu mwanzo, manabii waliokutangulia wewe na mimi walitabiri vita, maafa na tauni dhidi ya nchi nyingi na falme kubwa.
9
Lakini nabii atakayetabiri amani atatambuliwa kuwa kweli ametumwa na Bwana ikiwa unabii wake utatimia.”
10
Kisha nabii Hanania akaiondoa nira iliyokuwa shingoni mwa Yeremia na kuivunja,
11
naye akasema mbele ya watu wote, “Hili ndilo asemalo Bwana: ‘Vivi hivi ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadneza mfalme wa Babeli kutoka kwenye shingo za mataifa katika muda huu wa miaka miwili.’ ” Alipofanya hivi, nabii Yeremia akaondoka zake.
Settings