Skip to content
Yeremia 26:1-15

Yeremia 26:1-15

1
Mwanzoni mwa utawala wa Yehoyakimu mwana wa Yosia mfalme wa Yuda, neno hili lilikuja kutoka kwa Bwana:
2
“Hili ndilo Bwana asemalo: Simama katika ua wa nyumba ya Bwana na useme na watu wote wa miji ya Yuda wanaokuja kuabudu katika nyumba ya Bwana. Waambie kila kitu nitakachokuamuru, usipunguze neno.
3
Huenda watasikiliza, na kila mmoja akageuka kutoka njia yake mbaya. Kisha nitawahurumia na kuacha kuwaletea maafa niliyokuwa ninapanga kwa sababu ya maovu waliyofanya.
4
Waambie, ‘Hili ndilo asemalo Bwana: Ikiwa hamtanisikiliza na kuifuata sheria yangu ambayo nimeiweka mbele yenu,
5
nanyi ikiwa hamtayasikiliza maneno ya watumishi wangu manabii, ambao nimewatuma kwenu tena na tena (ijapokuwa hamkuwasikiliza),
6
ndipo nitaifanya nyumba hii kama Shilo na mji huu kuwa kitu cha kulaaniwa na mataifa yote ya dunia.’ ”
7
Makuhani, manabii na watu wote wakamsikia Yeremia akiyasema maneno haya ndani ya nyumba ya Bwana.
8
Lakini mara tu Yeremia alipomaliza kuwaambia watu kila kitu Bwana alichomwamuru kukisema, basi makuhani, manabii na watu wote walimkamata wakisema, “Ni lazima ufe!
9
Kwa nini unatoa unabii katika jina la Bwana kwamba nyumba hii itakuwa kama Shilo na mji huu utakuwa ukiwa na kuachwa tupu?” Nao watu wote wakamkusanyikia na kumzunguka Yeremia ndani ya nyumba ya Bwana.
10
Maafisa wa Yuda waliposikia kuhusu mambo haya, wakapanda kutoka jumba la kifalme, wakaenda katika nyumba ya Bwana na kushika nafasi zao kwenye ingilio la Lango Jipya la nyumba ya Bwana.
11
Kisha makuhani na manabii wakawaambia maafisa pamoja na watu wote, “Mtu huyu anastahili ahukumiwe kifo kwa sababu ametoa unabii mbaya dhidi ya mji huu. Mmesikia kwa masikio yenu wenyewe!”
12
Kisha Yeremia akawaambia maafisa wote na watu wote: “Bwana amenituma kutoa unabii dhidi ya nyumba hii na mji huu mambo yote mliyoyasikia.
13
Sasa tengenezeni njia zenu na matendo yenu, na kumtii Bwana Mungu wenu. Ndipo Bwana atawahurumia na kuacha kuleta maafa aliyokuwa ameyatamka dhidi yenu.
14
Lakini kwa habari yangu mimi, niko mikononi mwenu, nifanyieni lolote mnaloona kuwa ni jema na la haki.
15
Hata hivyo, jueni kwa hakika, ikiwa mtaniua, mtakuwa mmejipatia dhambi kwa damu isiyo na hatia juu yenu wenyewe, na juu ya mji huu na wote wanaoishi ndani yake, kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu ili niseme maneno haya yote masikioni mwenu.”
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options