Skip to content
Yeremia 23:21-40

Yeremia 23:21-40

21
Mimi sikuwatuma manabii hawa, lakini bado wamekimbia wakitangaza ujumbe wao. Mimi sikusema nao, lakini wametabiri.
22
Lakini kama wangesimama barazani mwangu, wangetangaza maneno yangu kwa watu wangu, nao wangewageuza kutoka njia zao mbaya na kutoka matendo yao maovu.”
23
“Je, mimi ni Mungu aliyeko hapa karibu tu,” Bwana asema, “wala si Mungu aliyeko pia mbali?
24
Je, mtu yeyote aweza kujificha mahali pa siri ili nisiweze kumwona?” Bwana asema. “Je, mimi sikuijaza mbingu na nchi?” Bwana asema.
25
“Nimesikia wanayoyasema manabii, hao wanaotabiri uongo kwa jina langu. Wanasema, ‘Nimeota ndoto! Nimeota ndoto!’
26
Mambo haya yataendelea mpaka lini ndani ya mioyo ya hawa manabii wa uongo, ambao hutabiri maono ya uongo ya akili zao wenyewe?
27
Wanadhani ndoto wanazoambiana wao kwa wao zitawafanya watu wangu walisahau jina langu, kama baba zao walivyolisahau jina langu kwa kumwabudu Baali.
28
Mwache nabii aliye na ndoto aseme ndoto yake, lakini yule aliye na neno langu na aliseme kwa uaminifu. Kwa maana jani kavu lina uhusiano gani na ngano?” asema Bwana.
29
“Je, neno langu si kama moto,” asema Bwana, “na kama nyundo ivunjayo mwamba vipande vipande?
30
“Kwa hiyo, niko kinyume na manabii wanaoibiana maneno kana kwamba ni yangu,” asema Bwana.
31
“Naam, mimi niko kinyume na manabii wanaotikisa ndimi zao wenyewe na kusema, ‘Bwana asema.’
32
Kweli, niko kinyume na hao wanaotabiri ndoto za uongo,” asema Bwana. “Wanazisimulia na kuwapotosha watu wangu kwa uongo wao bila kujali, lakini sikuwatuma wala sikuwaamuru. Hawawafaidi watu hawa hata kidogo,” asema Bwana.
33
“Wakati watu hawa, au nabii, au kuhani watakapokuuliza, ‘Mzigo wa Bwana ni nini?’ wewe utawaambia, ‘Ninyi ndio mzigo. Nami nitawavua kama vazi, asema Bwana.’
34
Nabii, kuhani, au mtu yeyote akisema, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ nitamwadhibu huyo na nyumba yake.
35
Hivyo mnaambiana kila mmoja na mwenzake, au kwa mtu wa nyumba yao: ‘Bwana amejibu nini?’ au ‘Bwana amesema nini?’
36
Lakini kamwe msiseme tena, ‘Nina mzigo wa Bwana,’ kwa sababu kila neno la mtu binafsi linakuwa mzigo wake mwenyewe, na hivyo kupotosha maneno ya Mungu aliye hai, Bwana Mwenye Nguvu Zote, Mungu wetu.
37
Hivi ndivyo utakavyoendelea kumuuliza nabii: ‘Bwana amekujibu nini?’ au ‘Je, Bwana amesema nini?’
38
Ingawa unadai, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ hili ndilo Bwana asemalo: Ulitumia maneno, ‘Huu ndio mzigo wa Bwana,’ hata ingawa nilikuambia kuwa kamwe usiseme, ‘Huu ni mzigo wa Bwana.’
39
Kwa hiyo, hakika nitakusahau na kukutupa mbali na uso wangu pamoja na mji niliowapa ninyi na baba zenu.
40
Nitaleta juu yako fedheha ya kudumu: yaani aibu ya kudumu ambayo haitasahaulika.”
Settings

Reading style

Typeface

Font size 19px

Reading width 75 chars

Options