Yeremia 2:20-28
20
“Zamani nilivunja nira yako na kukatilia mbali vifungo vyako; ukasema, ‘Sitakutumikia!’ Naam kweli, kwenye kila kilima kirefu na chini ya kila mti uliotanda matawi yake ulijilaza kama kahaba.
21
Nilikupanda ukiwa mzabibu ulio bora sana, mkamilifu na wa mbegu nzuri. Ilikuwaje basi ukawa kinyume nami, ukaharibika na kuwa mzabibu mwitu?
22
Hata ujisafishe kwa magadi na kutumia sabuni nyingi, bado doa la hatia yako liko mbele zangu,” asema Bwana Mwenyezi.
23
“Wawezaje kusema, ‘Mimi si najisi, sijawafuata Mabaali’? Kumbuka jinsi ulivyotenda kule bondeni; fikiri uliyoyafanya. Wewe ni ngamia jike mwenye mbio ukikimbia hapa na pale,
24
punda-mwitu aliyezoea jangwa, anayenusa upepo katika tamaa yake kubwa: katika wakati wake wa kuhitaji mbegu ni nani awezaye kumzuia? Madume yoyote yanayomfuatilia hayana haja ya kujichosha; wakati wa kupandwa kwake watampata tu.
25
Usikimbie hadi miguu yako iwe haina viatu, na koo lako liwe limekauka. Lakini ulisema, ‘Haina maana! Ninaipenda miungu ya kigeni, nami lazima niifuatie.’
26
“Kama vile mwizi aaibikavyo wakati amekamatwa, hivyo ndivyo nyumba ya Israeli inavyoaibishwa: wao wenyewe, wafalme wao na maafisa wao, makuhani wao na manabii wao.
27
Wanaiambia miti, ‘Wewe ndiwe baba yangu,’ nalo jiwe, ‘Wewe ndiwe uliyenizaa.’ Wamenipa visogo vyao wala hawakunigeuzia nyuso zao; lakini wakiwa katika taabu, wanasema, ‘Njoo utuokoe!’
28
Iko wapi basi ile miungu mliyojitengenezea? Yenyewe na ije kama inaweza kuwaokoa wakati mko katika taabu! Kwa maana mna miungu mingi kama mlivyo na miji, ee Yuda.
Settings