Skip to content
Yeremia 17:1-11

Yeremia 17:1-11

1
“Dhambi ya Yuda imechorwa kwa kalamu ya chuma, imeandikwa kwa ncha ya almasi, kwenye vibao vya mioyo yao na kwenye pembe za madhabahu zao.
2
Hata watoto wao wanakumbuka madhabahu zao na nguzo za Ashera, kandokando ya miti iliyotanda na juu ya vilima virefu.
3
Mlima wangu katika nchi pamoja na utajiri na hazina zako zote nitazitoa ziwe nyara, pamoja na mahali pako pa juu pa kuabudia miungu kwa sababu ya dhambi katika nchi yako yote.
4
Kwa kosa lako mwenyewe utaupoteza urithi niliokupa. Nitakufanya mtumwa wa adui zako katika nchi usiyoijua, kwa kuwa umeiwasha hasira yangu, nayo itawaka milele.”
5
Hili ndilo asemalo Bwana: “Amelaaniwa yeye amtegemeaye mwanadamu, ategemeaye mwenye mwili kwa ajili ya nguvu zake, ambaye moyo wake umemwacha Bwana.
6
Atakuwa kama kichaka cha jangwani; hataona mafanikio yatakapokuja. Ataishi katika sehemu zisizo na maji, katika nchi ya chumvi ambapo hakuna yeyote aishiye humo.
7
“Lakini amebarikiwa mtu ambaye tumaini lake ni katika Bwana, ambaye matumaini yake ni katika Bwana.
8
Atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji uenezao mizizi yake karibu na kijito cha maji. Hauogopi wakati wa joto ujapo; majani yake ni mabichi daima. Hauna hofu katika mwaka wa ukame na hautaacha kuzaa matunda.”
9
Moyo ni mdanganyifu kuliko vitu vyote, ni mwovu kupita kiasi. Ni nani awezaye kuujua?
10
“Mimi Bwana huchunguza moyo na kuzijaribu nia, ili kumlipa mtu kwa kadiri ya mwenendo wake, kwa kadiri ya matendo yake yanavyostahili.”
11
Kama kware aanguaye mayai asiyoyataga, ndivyo alivyo mtu apataye mali kwa njia zisizo za haki. Maisha yake yafikapo katikati, siku zitamwacha, na mwishoni atabainika kuwa mpumbavu.
Settings

Reading Style

Typeface

Font Size 19px

Options