Yeremia 1:4-19
4
Neno la Bwana lilinijia, kusema,
5
“Kabla sijakuumba ndani ya tumbo la mama yako, nilikujua; kabla hujazaliwa nilikutenga kwa kazi maalum; nilikuweka uwe nabii kwa mataifa.”
6
Nami nikasema, “Aa, Bwana Mwenyezi, sijui kusema, kwani mimi ni mtoto mdogo tu.”
7
Lakini Bwana akaniambia, “Usiseme, ‘Mimi ni mtoto mdogo tu.’ Utaenda popote nitakapokutuma na kunena lolote nitakalokuagiza.
8
Usiwaogope, kwa maana niko pamoja nawe nikuokoe,” asema Bwana.
9
Kisha Bwana akaunyoosha mkono wake na kugusa kinywa changu, akaniambia, “Sasa nimeyaweka maneno yangu kinywani mwako.
10
Tazama, leo nimekuweka juu ya mataifa na falme ili kungʼoa na kubomoa, kuharibu na kuangamiza, kujenga na kupanda.”
11
Neno la Bwana likanijia kusema, “Je, Yeremia unaona nini?” Nami nikajibu, “Naona tawi la mti wa mlozi.”
12
Bwana akaniambia, “Umeona vyema kwa maana ninaliangalia neno langu ili kuona kwamba limetimizwa.”
13
Neno la Bwana likanijia tena, “Unaona nini?” Nikajibu, “Naona chungu kinachochemka, kikiwa kimeinama kutoka kaskazini.”
14
Bwana akaniambia, “Kutoka kaskazini maafa yatamwagwa kwa wote waishio katika nchi.
15
Nitawaita watu wote wa falme za kaskazini,” asema Bwana. “Wafalme wao watakuja na kuweka viti vyao vya enzi katika maingilio ya malango ya Yerusalemu, watakuja dhidi ya kuta zake zote zinazouzunguka, na dhidi ya miji yote ya Yuda.
16
Nitatoa hukumu zangu kwa watu wangu kwa sababu ya uovu wao wa kuniacha mimi, kwa kufukiza uvumba kwa miungu mingine na kuabudu kile ambacho mikono yao imekitengeneza.
17
“Jiandae! Simama useme chochote nitakachokuamuru. Usiwaogope, la sivyo nitakufanya uwaogope wao.
18
Leo nimekufanya mji wenye ngome, nguzo ya chuma, na ukuta wa shaba ili kusimama dhidi ya nchi yote: dhidi ya wafalme wa Yuda, maafisa wake, makuhani wake na watu wa nchi hiyo.
19
Watapigana nawe lakini hawatakushinda, kwa kuwa niko pamoja nawe, nami nitakuokoa,” asema Bwana.
Settings