Isaya 5:8-25
8
Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.
9
Bwana Mwenye Nguvu Zote amesema nikisikia: “Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa, nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.
10
Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja ya divai, na homeri ya mbegu zilizopandwa itatoa efa moja tu ya nafaka.”
11
Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema wakikimbilia kunywa vileo, wale wakawiao sana mpaka usiku, mpaka wamewaka kwa mvinyo.
12
Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao, matari, filimbi na mvinyo, lakini hawayajali matendo ya Bwana, wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.
13
Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni kwa sababu ya kukosa ufahamu, watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa na watu wao wengi watakauka kwa kiu.
14
Kwa hiyo kaburi limeongeza hamu yake na kupanua mdomo wake bila kikomo, ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu, pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote.
15
Hivyo mwanadamu atashushwa, na binadamu kunyenyekezwa, macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.
16
Lakini Bwana Mwenye Nguvu Zote atatukuzwa kwa ajili ya haki yake, naye Mungu Mtakatifu atajionyesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa haki yake.
17
Kondoo watajilisha kwenye malisho yao wenyewe, wana-kondoo watajilisha katika magofu ya matajiri.
18
Ole wao wanaovuta dhambi kwa kamba za udanganyifu na uovu kama kwa kamba za mkokoteni,
19
kwa wale wanaosema, “Mungu na afanye haraka, aharakishe kazi yake ili tupate kuiona. Huo mpango wa Aliye Mtakatifu wa Israeli na ukamilike, tena udhihirike ili tupate kuujua.”
20
Ole wao wanaoita ubaya ni wema, na wema ni ubaya, wawekao giza badala ya nuru, na nuru badala ya giza, wawekao uchungu badala ya utamu, na utamu badala ya uchungu.
21
Ole wao walio na hekima machoni pao wenyewe, na kujiona wenye akili machoni pao wenyewe.
22
Ole wao walio mashujaa kwa kunywa mvinyo, nao walio hodari katika kuchanganya vileo,
23
wale wanaoachilia wenye hatia kwa kupokea hongo, lakini huwanyima haki wasio na hatia.
24
Kwa hiyo, kama ndimi za moto zirambavyo nyasi, na kama vile majani makavu yazamavyo katika miali ya moto, ndivyo mizizi yao itakavyooza na maua yao yatakavyopeperushwa kama mavumbi; kwa kuwa wameikataa sheria ya Bwana Mwenye Nguvu Zote na kulisukumia mbali neno la Aliye Mtakatifu wa Israeli.
25
Kwa hiyo hasira ya Bwana inawaka dhidi ya watu wake, mkono wake umeinuliwa na anawapiga. Milima inatetemeka, maiti ni kama takataka kwenye barabara. Hata kwa haya yote, hasira yake haijageukia mbali, mkono wake bado umeinuliwa juu.
Settings