Isaya 5:1-15
1
Nitaimba wimbo kwa ajili ya mmoja nimpendaye, kuhusu shamba lake la mizabibu: Mpendwa wangu alikuwa na shamba la mizabibu kwenye kilima chenye rutuba.
2
Alililima na kuondoa mawe na akaliotesha mizabibu bora sana. Akajenga mnara wa ulinzi ndani yake, na kutengeneza shinikizo la kukamulia divai pia. Kisha akatazamia kupata mazao ya zabibu nzuri, lakini lilizaa matunda mabaya tu.
3
“Basi enyi wakazi wa Yerusalemu na watu wa Yuda, hukumuni kati yangu na shamba langu la mizabibu.
4
Ni nini zaidi ambacho kingeweza kufanyika kwa shamba langu la mizabibu kuliko yale niliyofanya? Nilipotazamia kupata zabibu nzuri, kwa nini lilizaa zabibu mbaya tu?
5
Sasa nitawaambia lile nitakalolitendea shamba langu la mizabibu: Nitaondoa uzio wake, nalo litaharibiwa, nitabomoa ukuta wake, nalo litakanyagwa.
6
Nitalifanya nchi ya ukiwa isiyokaliwa na watu, halitakatiwa matawi wala kulimwa, nayo michongoma na miiba itamea huko, nitaamuru mawingu yasinyeshe mvua juu yake.”
7
Shamba la mzabibu la Bwana Mwenye Nguvu Zote ni nyumba ya Israeli, na watu wa Yuda ni bustani yake ya kumpendeza. Alitazamia haki, lakini akaona umwagaji damu, alitazamia uadilifu, lakini akasikia vilio vya taabu.
8
Ole wenu mnaoongeza nyumba baada ya nyumba na kuunganisha mashamba baada ya mashamba hadi hakuna nafasi iliyobaki, nanyi mnaishi peke yenu katika nchi.
9
Bwana Mwenye Nguvu Zote amesema nikisikia: “Hakika nyumba kubwa zitakuwa ukiwa, nayo majumba ya fahari yatabaki bila kukaliwa.
10
Shamba la mizabibu la eka kumi litatoa bathi moja ya divai, na homeri ya mbegu zilizopandwa itatoa efa moja tu ya nafaka.”
11
Ole wao wale waamkao asubuhi na mapema wakikimbilia kunywa vileo, wale wakawiao sana mpaka usiku, mpaka wamewaka kwa mvinyo.
12
Wana vinubi na zeze kwenye karamu zao, matari, filimbi na mvinyo, lakini hawayajali matendo ya Bwana, wala hawana heshima kwa ajili ya kazi ya mikono yake.
13
Kwa hiyo watu wangu watakwenda uhamishoni kwa sababu ya kukosa ufahamu, watu wao wenye vyeo watakufa kwa njaa na watu wao wengi watakauka kwa kiu.
14
Kwa hiyo kaburi limeongeza hamu yake na kupanua mdomo wake bila kikomo, ndani mwake watashuka wakuu wao na wingi wa watu, pamoja na wagomvi wao, na wafanyao sherehe wote.
15
Hivyo mwanadamu atashushwa, na binadamu kunyenyekezwa, macho ya wenye majivuno yatanyenyekezwa.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings