Isaya 49:1-13
1
Nisikilizeni, enyi visiwa, sikieni hili, ninyi mataifa mlio mbali: Kabla sijazaliwa, Bwana aliniita, tangu kuzaliwa kwangu, amelitaja jina langu.
2
Akafanya kinywa changu kuwa kama upanga ulionolewa, katika uvuli wa mkono wake akanificha; akanifanya kuwa mshale uliosuguliwa, na kunificha katika podo lake.
3
Akaniambia, “Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika yeye nitaonyesha utukufu wangu.”
4
Lakini nilisema, “Nimetumika bure, nimetumia nguvu zangu bure bila faida. Hata hivyo linalonistahili liko mkononi mwa Bwana, nao ujira wangu uko kwa Mungu wangu.”
5
Sasa Bwana asema: yeye aliyeniumba tumboni kuwa mtumishi wake, kumrudisha tena Yakobo kwake na kumkusanyia Israeli, kwa maana nimepata heshima machoni pa Bwana, naye Mungu wangu amekuwa nguvu yangu;
6
yeye asema: “Je, ni jambo dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kurejeza makabila ya Yakobo, na kuwarudisha wale Waisraeli niliowahifadhi? Pia nitakufanya uwe nuru kwa ajili ya watu wa Mataifa, ili upate kuleta wokovu wangu hata miisho ya dunia.”
7
Hili ndilo asemalo Bwana, yeye Mkombozi na Aliye Mtakatifu wa Israeli, kwake yeye aliyedharauliwa na kuchukiwa na taifa, kwa mtumishi wa watawala: “Wafalme watakuona na kusimama, wakuu wataona na kuanguka kifudifudi, kwa sababu ya Bwana, aliye mwaminifu, yeye Aliye Mtakatifu wa Israeli, aliyekuchagua wewe.”
8
Hili ndilo asemalo Bwana: “Wakati wangu uliokubalika nitakujibu, nami katika siku ya wokovu nitakusaidia; nitakuhifadhi, nami nitakufanya kuwa agano kwa ajili ya watu, ili kurudisha nchi na kugawanyia urithi tena wale waliokuwa ukiwa,
9
kuwaambia mateka, ‘Tokeni nje,’ nao wale walio gizani, ‘Kuweni huru!’ “Watajilisha kando ya barabara na kupata malisho yao juu ya kila kilima kilicho kitupu.
10
Hawataona njaa wala kuona kiu, wala hari ya jangwani au jua halitawapiga. Yeye mwenye huruma juu yao atawaonyesha njia, na kuwaongoza kando ya chemchemi za maji.
11
Nitaifanya milima yangu yote kuwa barabara, na njia kuu zangu zitainuliwa.
12
Tazama, watakuja kutoka mbali: wengine kutoka kaskazini, wengine kutoka magharibi, wengine kutoka nchi ya Sinimu.”
13
Pigeni kelele kwa furaha, enyi mbingu; furahi, ee dunia; pazeni sauti kwa kuimba, enyi milima! Kwa maana Bwana anawafariji watu wake, naye atakuwa na huruma kwa watu wake walioumizwa.
Settings