Isaya 44:1-8
1
“Lakini sasa sikiliza, ee Yakobo, mtumishi wangu, Israeli, niliyemchagua.
2
Hili ndilo asemalo Bwana, yeye aliyekuhuluku, aliyekuumba tumboni, yeye atakayekusaidia: Usiogope, ee Yakobo, mtumishi wangu, Yeshuruni, niliyekuchagua.
3
Kwa maana nitamimina maji juu ya nchi yenye kiu, na vijito vya maji juu ya ardhi iliyokauka; nitamimina Roho wangu juu ya watoto wako, nayo baraka yangu juu ya wazao wako.
4
Nao watachipua kama manyasi katika shamba la majani, kama mierezi kando ya vijito vya maji yatiririkayo.
5
Mmoja atasema, ‘Mimi ni wa Bwana’; mwingine atajiita kwa jina la Yakobo; vilevile mwingine ataandika juu ya mkono wake, ‘Wa Bwana,’ na kujiita kwa jina la Israeli.
6
“Hili ndilo asemalo Bwana, Mfalme wa Israeli na Mkombozi, Bwana Mwenye Nguvu Zote: Mimi ni wa kwanza na Mimi ni wa mwisho; zaidi yangu hakuna Mungu.
7
Ni nani basi aliye kama mimi? Yeye na atangaze. Yeye atangaze na kuweka mbele yangu ni kitu gani kilichotokea tangu nilipoumba watu wangu wa kale, tena ni nini kitakachotokea: naam, yeye na atoe unabii ni nini kitakachokuja.
8
Msitetemeke, msiogope. Je, sikutangaza hili, na kutoa unabii tangu zamani? Ninyi ni mashahidi wangu. Je, yuko Mungu zaidi yangu mimi? Hasha, hakuna Mwamba mwingine; mimi simjui mwingine.”
Settings