Isaya 24:10-23
10
Mji ulioharibiwa umekuwa ukiwa, mlango wa kila nyumba umefungwa.
11
Barabarani wanalilia kupata mvinyo, furaha yote imegeuka kuwa majonzi, furaha yote imefukuziwa mbali na dunia.
12
Mji umeachwa katika uharibifu, lango lake limevunjwa vipande.
13
Ndivyo itakavyokuwa duniani na miongoni mwa mataifa, kama vile wakati mzeituni upigwavyo, au kama vile wakati masazo yabakiavyo baada ya zabibu kuvunwa.
14
Wanainua sauti zao, wanapiga kelele kwa furaha, kutoka magharibi wanasifu kwa ukelele utukufu wa Bwana.
15
Kwa hiyo upande wa mashariki mpeni Bwana utukufu, liadhimisheni jina la Bwana, Mungu wa Israeli, katika visiwa vya bahari.
16
Kutoka miisho ya dunia tunasikia uimbaji: “Utukufu kwa Yule Mwenye Haki.” Lakini nilisema, “Ninadhoofika, ninadhoofika! Ole wangu! Watenda hila wanasaliti! Kwa hila watenda hila wanasaliti!”
17
Hofu, shimo na mtego vinakungojea, ewe mtu ukaaye duniani.
18
Kila akimbiaye asikiapo sauti ya hofu atatumbukia shimoni, naye yeyote apandaye kutoka shimoni, atanaswa kwenye mtego. Malango ya gharika ya mbinguni yamefunguliwa, misingi ya dunia inatikisika.
19
Dunia imepasuka, dunia imechanika, dunia imetikiswa kabisa.
20
Dunia inapepesuka kama mlevi, inayumbayumba kama kibanda kwenye upepo; imelemewa sana na mzigo wa hatia ya uasi wake na ikianguka kamwe haitainuka tena.
21
Katika siku ile Bwana ataadhibu nguvu zilizoko mbinguni juu, na wafalme walioko duniani chini.
22
Watakusanywa pamoja kama wafungwa waliofungwa gerezani, watafungiwa gerezani na kuadhibiwa baada ya siku nyingi.
23
Mwezi utatiwa haya, nalo jua litaaibishwa; kwa maana Bwana Mwenye Nguvu Zote atawala juu ya Mlima Sayuni na katika Yerusalemu, tena mbele ya wazee wake kwa utukufu.
Maandiko ya Biblia: Biblica® Open Kiswahili Contemporary Version (Neno: Bibilia Takatifu)™, © 1984, 1989, 2009, 2015 Biblica, Inc. · CC BY-SA 4.0“Biblica” is a trademark registered in the United States Patent and Trademark Office by Biblica, Inc., used with permission.
Settings