Isaya 17:1-11
1
Neno kuhusu Dameski: “Tazama, Dameski haitakuwa tena mji bali itakuwa lundo la magofu.
2
Miji ya Aroeri itaachwa na itaachiwa mifugo ambayo italala huko, bila yeyote wa kuyaogopesha.
3
Mji wenye ngome utatoweka kutoka Efraimu, nao uweza wa ufalme kutoka Dameski; mabaki ya Aramu yatakuwa kama utukufu wa Waisraeli,” asema Bwana Mwenye Nguvu Zote.
4
“Katika siku ile utukufu wa Yakobo utafifia, unono wa mwili wake utadhoofika.
5
Itakuwa kama mvunaji akusanyavyo nafaka na kuvuna nafaka kwa mikono yake, kama wakati mtu aokotapo masazo ya masuke katika Bonde la Warefai.
6
Hata hivyo baadhi ya masazo yatabaki, kama vile mti wa mzeituni unavyopigwa, kukiachwa zeituni mbili au tatu juu ya matawi kileleni, nne au tano katika matawi yazaayo sana,” asema Bwana, Mungu wa Israeli.
7
Katika siku ile watu watamwangalia Muumba wao, na kuelekeza macho yao kwa yule Aliye Mtakatifu wa Israeli.
8
Hawataziangalia tena madhabahu, kazi za mikono yao, nao hawataheshimu nguzo za Ashera, na madhabahu za kufukizia uvumba zilizofanywa kwa mikono yao.
9
Katika siku ile miji yao iliyo imara, ambayo waliihama kwa sababu ya Waisraeli, itakuwa kama mahali palipoachwa pa vichaka na magugu. Nayo yote itakuwa ukiwa.
10
Mmemsahau Mungu Mwokozi wenu, hamkumkumbuka Mwamba aliye ngome yenu. Kwa hiyo, hata ingawa mlipandikiza mimea iliyo mizuri sana na kuotesha mizabibu ya kigeni,
11
hata kama siku ile unapoipandikiza, unaifanya iote na asubuhi ile ile unayoipanda, unaifanya ichipue, hata hivyo mavuno yatakuwa kama si kitu katika siku ile ya ugonjwa na maumivu yasiyoponyeka.
Settings